Serikali kupitia Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu imekuwa ikiajiri askari waliohitimu Astashahada ya Wanyamapori, Misitu pamoja na Askari waliohitimu Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa ajili ya kulitumikia Jeshi la Uhifadhi nchini
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Malinyi, Mhe. Antipas Mgungusi aliyetaka kujua lini Serikali itawatumia vijana ambao wamepata mafunzo ya JKT katika kulitumikia Jeshi la Uhifadhi kwa mkataba wa muda mfupi.
“Kutokana na upungufu mkubwa wa watumishi hususan askari, SUMA JKT wamekuwa wakiingia mikataba ambayo inawezesha vijana waliohitimu JKT kupata kazi za mikataba kwa shughuli mbalimbali za ulinzi wa maliasili kama wanyamapori na misitu” Mhe. Masanja amesisitiza akitolea mfano wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ambayo imeingia mkataba na SUMA JKT kwa ajili ya kuongeza nguvu ya ulinzi wa misitu kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa wa askari.
Aidha, Mhe. Masanja amesema kuwa Serikali imekuwa ikiwatumia vijana wa JKT walioko makambini kwa ajili ya doria za muda mfupi zinapotokea changamoto za wanyama wakali na waharibifu.
Akijibu swali la Mbunge wa Ushetu , Mhe. Emmanuel Cherehani aliyetaka kujua lini Serikali itamaliza Mgogoro wa mpaka wa Pori la Usumbwa Forest Reserve na Hifadhi ya Pori la Kigosi Moyowosi katika Jimbo la Ushetu, Mhe. Masanja amesema kuwa hakuna mgogoro katika Pori hilo na wananchi, bali wananchi waliomba kupatiwa eneo ambapo Serikali inaendelea na tathmini na pindi itakapokamilika wananchi watajulishwa.
“Nataka niwaambie wanachi wa Ushetu kwamba tunaangalia utaratibu wa kuyashusha hadhi baadhi ya maeneo ili wananchi waendelee kupata faida ya uhifadhi na pia waendelee na shughuli za ufugaji nyuki” Mhe. Masanja amesema.
Kuhusu ukarabati wa majengo ya Magofu ndani ya Mji Mkongwe wa Bagamoyo, Mhe. Masanja amesema Wizara imeendelea kuwahamasisha wadau wote kufanya ukarabati usioathiri mwonekano au kuharibu historia hiyo.
Aidha, amesema Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ipo katika mpango wa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Ngome Kongwe baada ya kufanyiwa uokoaji (rescue) kwa kuliimarisha jengo hilo.