Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo amekemea tabia ya kupunguza fidia kwa wananchi walioathiriwa na wanyama wanaotoka hifadhini na kusema hali hiyo inatengeneza chuki kati ya Chama,Serikali na Wananchi kwa ujumla.
Chongolo amekemea vitendo hivyo,leo kufuatia malalamiko ya wananchi wa Kata ya Itaswi Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma wanapakana na Hifadhi ya Tarangire na Pori la Akiba la Mkunganero ambao wamelalamika juu ya kupewa fidia sawa bila kufanyika tathmini ya usawa juu ya athari iliyopatikana.
Akizungumza baada ya kushiriki mkutano wa Shina namba sita katika tawi la Itaswi amesema kinachofanywa na baadhi ya Ofisi za
Wakurugenzi wa Halmashauri za kuidhinisha fidia ndogo kwa waathirika ni ubinafsi na kuwataka watengeneza mazingira mazuri ya kutenda haki kwa wananchi walioathiriwa na wanyama kutoka hifadhini.
Awali akizungumzia katika mkutano huo, ABED DURU ambaye ni mwananchi wa Kata ya Itaswi amelalamikia kuharibiwa kwa mazao yao na wanyama wanaotoka katika Hifadhi ya Tarangire na pori la Akiba la Mkunganero,lakini kumekuwa na ucheleweshwaji mkubwa wa fidia ambayo pia imekuwa haiendani na kiwango cha uharibifu.
Kutokana na hilo Chongolo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kondoa kuchukua idadi ya walioathiriwa na wanyama kutoka hifadhini na kulipwa kwa wakati na kwa usahihi.
Flovarica Kalambo ni Afisa Mhifadhi kutoka Pori la Akiba Mkunganero ambaye amesema kwa sasa wanaandaa mafunzo maalumu watakaotoa elimu kwa wananchi jinsi ya kukabiliana na uvamizi wa wanyama kutoka Hifadhini.
Haya yamejiri katika mfululizo wa Ziara ya Katibu Mkuu aliyeambatana na Katibu wa NEC-Itikadi na Uenezi Sophia Mjema na Katibu wa NEC-Oganaizesheni Issa Haji Gavu ambapo leo wapo katika Wilaya ya Kondoa.