Na. Majid Abdulkarim -Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya itagharamia matibabu ya Watoto 20 wenye ugonjwa wa Sikoseli kwa kupandikizwa Uroto katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Benjamini Mkapa (BMH) bila malipo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo tarehe 19 June 2023, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sikoseli Duniani ambapo Kitaifa yamefanyika katika kituo cha afya Makole Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Shilingi Bilioni 5 kugharamia huduma za ubingwa bobezi ikiwemo upandikizaji wa uroto kwa watoto wenye sikoseli 20, hivyo amewataka wataalam wa upandikizaji huo kujiandaa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
“Mwaka huu naomba wazazi au walezi ambao mna watoto muwapeleke Hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na nimetoa changamoto kwa Benjamin Mkapa wapandikize watoto 20 ambao watadhaminiwa kwa asilimia 100 na Rais Samia Suluhu Hassan, hakutakuwa na kuchangia”. Ameeleza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Wizara ya Afya zaidi ya Shilingi bilioni 5 kwa ajili ya huduma za ubingwa bobezi ikiwemo kupandikiza uroto kwa watoto 20.
“Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuhakikisha huduma za upandikizaji uloto zinapatikana kwa watoto wengi ndo maana Mheshimiwa Rais ameahidi atagharamia watoto 20 wenye ugonjwa wa Sikoseli kutokana na gharama zake kuwa juu”. Ameongeza Waziri Ummy.
Gharama za upandikizaji wa uroto kwa wagonjwa wa selimundu zinatajwa kuwa kati ya Shilingi milioni 55 kwa mgonjwa mmoja nchini wakati nje ya Nchi matibabu hayo ni Shilingi milioni 120 hadi 150.
Matibabu ya uroto uhusisha uvunaji, uchakataji, na upandikizaji wa chembe chembe hai mama za damu.
Hata hivyo amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye ugonjwa wa Sikoseli kuwapeleka kliniki wakafanyiwe uchunguzi kwani Serikali inataka kuona watoto wenye ugonjwa huo wanaishi bila kupata maambukizi ya bakteria, hawapungukiwi damu na maumivu ya mifupa.
Pia ametoa wito kwa wazazi kwenda kwenye kliniki za Sikoseli katika hospitali za rufaa za mikoa, kanda na vituo vya afya, hivyo mtu anaweza kuanzia katika kituo cha afya kama Makole (Dodoma) watakao waunganisha na Hospitali ya Benjamini Mkapa na Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mei 10 mwaka huu Hospitali ya BMH ilianza kutoa huduma ya kupandikiza uroto ambapo watoto watatu waishio na ugonjwa wa Sikoseli walipandikiziwa huduma hiyo.
Hospitali ya BMH ni hospitali ya pili nchini kutoa huduma hiyo muhimu baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambayo yenyewe ilianza kutoa huduma hiyo rasmi mwaka 2021.