Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema madhumuni ya ziara yake nchini Ujerumani ni kuhudhuria mwaliko wa mashindano ya Dunia ya Olimpiki Maalumu yaliyofunguliwa jana akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan.
Ameyasema hayo leo tarehe 18 Juni 2023 akizungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Ujerumani katika ukumbi wa Hoteli ya Berlin Mariott.
Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema uhusiano wetu na Ujerumani ni mzuri sana kwa heshima waliyotupa kutualika katika mashindano ya Dunia ya Olimpiki Maalumu.
Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali inaridhika sana na mchango wa wana Diaspora kwa maendeleo ya uchumi wa nchi kwa miamala ya fedha kwenda nchini, uwekezaji wa miradi mbalimbali.
Amesema Serikali imeleta mfumo wa usajili kwa watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa usajili wa kidijitali kwa utambuzi pia ipo tayari kupokea ujuzi na fani mbalimbali za watanzania waliojifunza katika nchi mbalimbali kwa kujenga uchumi wa nchi.
Dk.Mwinyi amewataka wana Diaspora kuisemea vema nchi na kuwa mabalozi kwa kuzitangaza fursa mbalimbali pia amewapa moyo waendelee kufanya uwekezaji , biashara nchini Tanzania na Serikali italinda mitaji yao.