Na. Zillipa Joseph, Katavi
Wazazi na walezi mkoani Katavi wametakiwa kuacha kulaza watoto wao na wageni kutokana na matukio mengi ya ukatili wa kingono dhidi ya watoto kufanywa katika ngazi ya familia.
Kwa mwaka 2022 jumla ya matukio 1,459 ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa; huku matukio 224 ni ya watoto wa umri wa chini ya miaka nane waliofanyiwa ukatili wa kingono katika ngazi ya familia.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Mpanda Bi. Jamila Yusuf wakati wakiadhimisha ya siku ya mtoto wa Afrika leo katika kijiji cha Mwamkulu kilichopo Manispaa ya Mpanda.
Bi. Jamila amesema utamaduni huo umepitwa na wakati na hauendani na dunia ya sasa kwani binadamu wamebadilika sana tabia na kuacha kuwa waaminifu.
‘Anapokuja mgeni kama huna chumba mtandikie sebuleni alale. Na kama una watoto wengi jenga mazoea ya kuwakagua mara kwa mara maana wengine wanafanyiwa vitendo hivyo na ndugu wao wa damu’ alisema.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Katavi aliye safarini kikazi, Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu alisema kwa mwaka huu pekee ni matukio 46 tu yaliyoripotiwa mpaka sasa na kuitaka jamii kuacha kuficha kwani kwa kufanya hivyo kunawaathiri watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono kisaikolojia.
‘Ukilinganisha takwimu za mwaka uliopita na sasa hata kama hatujamaliza mwaka tofauti ni kubwa sana, hivyo niitake jamii isifiche haya mambo’ alisema Buswelu.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Katavi bwana Wilson Kennedy alisema watoto wanaokumbwa na kadhia hiyo wanapatiwa huduma za malezi na msaada wa kisaikolojia.
Hata hivyo ameongeza kuwa baadhi ya familia zinaficha ukweli kutokana na matendo hayo kufanywa na wanafamilia hali inayosababisha watoto wanaofanyiwa ukatili wa kingono kuathirika kisaikolojia.
Aidha kuhusu watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi, jumla ya watoto 374 walipata elimu ya kujikinga na maambukizi mapya huku watoto 292 walipata elimu ya ufuasi mzuri wa dawa.
Kwa upande wao watoto wametaja changamoto wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na utelekezwaji pale wazazi wanapotengana, kupigwa na kubakwa.