Mtaalamu wa sheria za kimataifa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SAUT Mwanza Balozi Profesa Costa Rick Mahalu akizungumza na wadau wa Sheria wakati akiwasilisha mada ya fikra na falsafa kwa wanasheria katika muhadhara wa wadau hao uliofanyika Ukumbi wa sheikh Idriss Abdul- wakil Kikwajuni Zanzibar.Juni 17,2023. PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR.
Wadau wa Sheria wakifuatilia mhadhara wa Sheria uliofanyika ukumbi wa sheikh Idris Abdul-Wakil Kikwajuni Mjini Unguja.
Naibu kadhi mkuuu Zanzibar Sheikh Othman Ame Chum Bakar akichangia mada katika mhadhara wa wadau wa sheria uliofanyika Ukumbi wa sheikh Idriss Abdul wakil Kikwajuni Zanzibar.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) na Mjumbe wa Baraza la skuli ya Sheria Profesa mohammed Makame Haji akichangia mada katika mhadhara wa wadau wa Sheria uliofanyika Ukumbi wa sheikh Idriss Abdul wakil Kikwajuni Zanzibar.
Mwanafunzi wa Skuli ya Sheria Zanzibar Deva F.Urio akichangia mada katika mhadhara wa wadau wa sheria uliofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil Kikwajuni Mjini Unguja.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) na Mjumbe wa Baraza la skuli ya Sheria Profesa mohammed Makame Haji akizungumza na wadau wa sheria wakati alipokua akifunga mhadhara wa wadau hao ulihusiana na masuala ya kisheria na kufanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul wakil Kikwajuni Mjini Unguja.
…………….
NA KHAMISUU ABDALLAH.
MAJAJI, Mahakimu na watendaji wote wanaosimamia sheria Zanzibar, wametakiwa kuhakikisha wanatenda haki katika utekelezaji wa kazi zao za kila siku katika kuihudumia jamii.
Mtaalamu wa Sheria za Kimataifa, Balozi Proffesa Costa Rick Mahalu, alieleza hayo wakati akiwasilisha mada ya Fikra na falsafa kwa wanasheria katika mhadhara wa maadili ya wanasheria uliowajumiisha majaji, makadhi,mahakimu, Mawakili wa umma na Mawakili wa kujitegemea uliofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul- Wakil Kikwajuni.
Alisema ni lazima matendo yao kama viongozi kutenda haki pale wanapotekeleza majukumu yao.
Alisema ni lazima kuona haki inatendeka kuona jamii wanayoihudumia haiwaonei katika kutekeleza wajibu wao wanapokuwepo katika vyombo vya sheria.
Sambamba na hayo, aliwataka watendaji hao wakiwemo wanataaluma, watafiti wa vyuo vikuu, mahakimu, majaji, wanasheria na wanataaluma wengine kuhakikisha wanafanya tafiti mbalimbali ambazo zitaisaidia jamii kufahamu na kuona haki wanayoitenda inajulikana moja kwa moja.
“Kufanya utafiti ni jambo la lazima na unapojifunza sheria kwa kingereza unakuwa ni mtumwa hivyo ni lazima kufanya utafiti na kuzifahamu taratibu za jamii katika maisha yao na kuweza kuzitumia,” alisisitiza.
Mbali na hayo, aliwasisitiza kukuza lugha yao ya kiswahili sanifu katika kuendesha mashauri yaomahakamani na kuyaandika kwa lugha hiyo kwani inatambulika duniani kote.
“Kiswahili tukipe kipaumbele na sheria zetu ziwe kwa lugha ya kiswahili hatua hiii itawezesha kukuza lugha yetu na kuwapa fursa wananchi kujua sheria mbalimbali kwa lugha hiyo kuliko lugha ya kingereza ambayo inawanyima fursa wananchi kufahamu,” alibainisha.
Hata hivyo, aliupongeza uongozi wa skuli ya sheria kwa kuamua kumpa nafasi hiyo ambayo itawasaidia viongozi hao wanaosimamia sheria Zanzibar kuwajibika ipasavyo.
Naye Mkuu wa Chuo cha Sheria Zanzibar, Dk. Ali Ukki, alisema lengo la Mhadhara huo ni kuzijengea uwezo tasisi za sheria nchini kuhakikisha zinatenda haki kwa jamii inayowazunguka.
Alisema ni lazima majaji, Mawakili na makadhi kuwasaidia kutanua wigo wa kufanya maamuzi na majaji kuweza kujenga hoja ili kuweza kufikia maamuzi mazuri katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mapema Jaji wa Mahakama kuu Zanzibar, Mummin Khamis Kombo, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa maendeleo ya fani ya sheria Zanzibar.
Alisema fani ya sheria ni muhimu kwani awali fani hiyo walikuwa wakikosa elimu ya fikra na falsafa kwani ushauri ni muhimu kwa fani hiyo hasa namna ya kufikiri katika kutekeleza kazi zao.
Aidha alibainisha kuwa ni vyema kuzingatia jambo hilo ili kuleta ufanisi kwani mahakama ni moyo na makuzi ya sheria za Zanzibar ili kuona hazipotoshwi.
Hata hivyo, alisema mawakili pia wana jukumu la kusaidia mahakama kutenda haki hasa katika kesi wanazoziendesha kwa kujua matumizi sahihi ya sheria zilizopo.
Nao washiriki wa mhadhara huo waliipongeza skuli ya sheria Sheria kwa kuwapa elimu iliyowanufaisha nakuwafanya wanasheria kufikiria kwa undani zaidi kwa kuangalia mazingira na sera za nchi ikiwemo Uchumi wa bluu.
“Mafunzo haya yanatufanya kufikiria kwa vitendo na fikra zetu ziweze kufikiria mambo mengine ikiwemo Uchumi, ulinzi na mambo ya kijamii ili kutoa haki kwa usahihi,” alisema.
Walisema kwenye mahakama ya kadhi kuna umuhimu mkubwa wa kufikiri na kufahamu kuliko mahakama nyengine za kawaida.