Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo, ametaka kuchukuliwa hatua za haraka katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma kwa kuwa hali ikiachwa hivyo itatishia uwepo wa ukame.
Chongolo amelazimika kutoa kauli hiyo Mjini Mpwapwa katika mkutano wa ndani wa hitimisho la ziara yake katika wilaya ya Mpwapwa, alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali wilayani humo.
Katika kukabiliana na hali hiyo Katibu Mkuu huyo wa CCM aliyeambatana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema pamoja na Katibu wa NEC, Oganaizesheni , Issa Haji Gavu, amesema hali inatisha wilayani Mpwapwa kwa uharibifu wa mazingira vikiwemo vyanzo vya maji na misitu.
Hivyo ameutaka uongozi wa Mkoa wa Dodoma, wilaya ya Mpwapwa pamoja na kamati ya siasa ya CCM Wilaya Mpwapwa kuandaa kikao cha haraka cha pamoja kitakachokuja na majibu ya namna ya kumaliza tatizo la uharibifu huo wa mazingira.
Mpwapwa ambayo ina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya elfu saba ambayo ni sawa na asilimia 18 ya mkoa mzima wa Dodoma, eneo lake kubwa linahatarishwa kutokana na ukataji hovyo wa misitu unaofanywa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu wilayani humo.
Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inaonesha kuwa wilaya ya Mpwawa ina zaidi ya wananchi laki nne, hivyo eneo lake sehemu kubwa linakabiliwa na uharibifu wa mazingira na hivyo kuhatarisha uoto wa asili na kuwa ni hatari kwa wananchi.
Chongolo amesema miaka 10 iliyopita wilaya hiyo ya Mpwapwa ili kuwa na wingi wa vyanzo wa maji lakini sasa hali hiyo haipo na hivyo kuagiza hatua za haraka kuchukuliwa za kuhifadhi mazingira.
Kuhusu mradi wa Reli ya kisasa SGR, Mtendaji huyo mkuu wa chama tawala amesisitiza kuwa mradi huo wenye uwekezaji hadu sasa wa zaidi ya Trilioni 7, hautakwama kama inavyodaiwa na watu wasio na mapenzi mema ya nchi.
Katika mradi huo wa SGR, tayari serikali imeshaleta mabehewa sita ya ghorofa kati ya mabehewa 30 yanayotakiwa kutumiwa na mradi huo. Na yaliyobaki yataletwa baadaye.
Akizungumzia tena kuhusu suala la Bandari ambalo limekuwa likipotoshwa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa nchini, Chongolo amesema dhamira ya serikali katika uwekezaji wa bandari ni njema katika majadiliano na kampuni ya DP world ambayo ni kampuni ya tatu kwa uwekezaji kwenye bandani duniani, hivyo serikali iendelee na majadiliano hayo ya ushirikiano yenye manufaa kwa taifa.
Chongolo, amesema chama hakiwezi kufanya jambo baya kwa taifa na wananchi kwa ujumla, hivyo wananchi waunge mkono juhudi za serikali katika kuwaletea maendeleo likiwemo suala ya bandari.