Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bw. Adam Fimbo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi wakibadilishana nyaraka wakati wa utiaji saini hati ya makubaliano kati ya MNH na TMDA ya kuimarisha ufuatiliaji wa maudhi, madhara au matukio yatokanayo na matumizi ya bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bw. Adam Fimbo akiungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bw. Adam Fimbo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi wakitiliana saini hati ya makubaliano kati ya MNH na TMDA ya kuimarisha ufuatiliaji wa maudhi, madhara au matukio yatokanayo na matumizi ya bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo
…………………
Na mwandishi wetu,
Dar es Salaam.
Hospitali ya Taifa Muhimbili imeongoza kitaifa kwa 57% katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo kwenye utoaji taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kati ya taarifa zote zilizopokelewa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa miaka ya fedha ya (2020/21,2021/22 na 2022/23.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Bw. Adam Fimbo wakati wa utiaji saini hati ya makubaliano kati ya MNH na TMDA ya kuimarisha ufuatiliaji wa maudhi, madhara au matukio yatokanayo na matumizi ya bidhaa zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.
Bw. Fimbo amesema, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imeweza kutumia fursa hiyo na kuwa taasisi inayoongoza kitaifa katika kuwasilisha taarifa za maudhi, madhara au matukio hayo. Hali hii imeimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizi mbili zenye nia moja ya kuboresha utoaji wa huduma za afya na kulinda afya ya jamii nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema pamoja na mambo mengine, makubaliano haya yanalenga kuimarisha mifumo ya utambuzi, ukusanyaji, utoaji taarifa za madhara ya dawa, chanjo, vitendanishi na vifaa tiba.
“Tunalenga kuboresha mifumo ya kubaini na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa kwenye soko zinazodhibitiwa na TMDA, kuimarisha mfumo wa usimamizi wa ubora, kuimarisha utoaji huduma bora za afya kwa kuzingatia viwango na ithibati za kimataifa,” ameongeza Prof. Janabi.