Na. WAF – Dodoma
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Serikali ya Namibia itaendelea kushirikiana kwa pamoja hasa katika sekta ya afya kwa kuwa nchi hizo mbili zimekuwa na historia nzuri ya kuimarisha mifumo ya afya.
Hayo ameyasema leo Juni 13, 2023 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa kikao na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Usawa wa Kijinsia, Maendeleo ya Jamii na Mambo ya Familia kutoka nchini Namibia kilichofanyika katika hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.
“Kwa kutambua urafiki wa nchi zote mbili, naamini urafiki wetu umekuwa na manufaa sana katika mfumo wa huduma za Afya wa Tanzania lakini pia tunakushukuru kwa kutembelea nchi yetu na ninaamini tutaendelea kuwa na uhusiano mzuri kwa kuwahudumia wananchi wetu.” Amesema Waziri Ummy
Aidha, katika kikao hicho Waziri Ummy na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Usawa wa Kijinsia, Maendeleo ya Jamii na Mambo ya Familia kutoka nchini Namibia wamejadiliana mambo mbalimbali yanayohusu afya ikiwemo masuala ya Ubora wa afya ya Umma, Utekelezaji wa mpango mkakati wa hali ya afya katika kupambana na magonjwa yakiwemo magonjwa yasiyoambukiza.
Pia, wamejadiliana hali ya upatikanaji wa huduma za afya na miundombinu, gharama ya huduma ya afya ya Umma kwa lengo la kujifunza na kuona huduma hizo zinavyotolewa Nchini Tanzania.
Katika upande wa upatikanaji wa huduma za afya na miundombinu Waziri Ummy amesema Huduma ya afya nchini Tanzania inatolewa kupitia mchanganyiko wa sekta za umma na binafsi ambapo Wizara ya Afya ina jukumu la kusimamia na kuratibu huduma za afya nchini.
“Hivi sasa hapa nchini tuna jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 11,040 ambavyo vinajumuisha vituo vya umma 6,682 na kwa utendaji kazi wake tuna Hospitali 430, vituo vya Afya 1,030, zahanati 1,458 na maabara za binafsi 1,206”. Amesema Waziri Ummy
Mwisho, Waziri Ummy amesema huduma za Afya ya Msingi imeimarishwa kwa kujenga miundombinu kwa kutumia ufadhili wa UVIKO-19 ikiwemo Idara za wagonjwa wa nje na za Dharura.