……………………………………………………….
Na Dotto Mwaibale, Aliyekuwa Geita.
WANANCHI wa Jimbo la Geita Vijijini wamesikitishwa na madai yanayotolewa na baadhi ya watu wakimhusisha Mbunge wao, Joseph Kashiku Musukuma na rushwa ya kununuliwa gari ili kutetea kupitishwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari mjini Geita, wananchi hao wametoa onyo na tahadhari kwa watu hao waliopo ndani na nje ya nchi kuwa waache kufanya hivyo wakimtaja Musukuma kuwa ni kiongozi muadilifu kutokana na uzalendo alionao hivyo hawezi kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Boniface Mkongo mkazi wa Kata ya Nkome katika jimbo hilo, alisema kwa muda ambao Musukuma amewatumikia katika nafasi mbalimbali kuanzia udiwani,uenyekiti wa Halmashauri, uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita na sasa Mbunge amekuwa kiongozi mwadilifu na mchapakazi na kuwa walioanza kumchafua wanatumika ili kumpunguza kasi ya kupambana na mafisadi na kuwa wanaofanya hivyo wanatumwa na watu wanaonyemelea jimbo hilo.
“Hawa wanaoanzisha chokochoko hizi wanatumika kisiasa kwa lengo la kumrudisha nyuma na hawata fanikiwa hata kidogo watuachie mbunge wetu aendelee kututumikia tunaamini kuwa ndiye mbunge wetu wa maisha kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kutuletea maendeleo,” alisema Mkongo.
Nao Elias Masune na Anna Masune walisema hawakuwahi kuwaza kwamba Geita vijijini siku moja watakuja kupata umeme lakini kutokana na juhudi na kazi kubwa aliyoifanya mbunge wao imewezekana na hao walioanza kumchafua wanataka kumdhoofisha kisiasa ili asiendelee kuleta maendeleo jambo ambalo hawatakubali badala yake watapambana nao.
“Leo umeme tunao, barabara zetu zimewekwa lami na taa, wamepita wabunge wengi hakuna tulichoona sasa tumepata mbunge mwadilifu watu wameanza kumchafua,tunawajua na njama zao tunazijua tunawapa onyo waache mara moja kufanya hivyo,” alisema Elias Masune.
Mwananchi mwingine Pius Manoni alisema mbunge wao ni mtu mwadilifu na pia ni mfanyabiashara anayejitosheleza kifedha hivyo hawezi kushawishika na rushwa ya kununuliwa gari la Sh.milioni 500 kama inavyodaiwa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii.
“Mbunge wetu ameanza kumiliki magari ya kifahari hata kabla hajawa mbunge na fedha zake anazipata kutokana na biashara zake na uwekezaji kwenye madini, nyumba, kilimo na ufugaji hivyo kununa kitu cha shilingi milioni 500 ni pesa ndogo sana kwake,” alisema Tongatuje Mawenge.
Wananchi hao walisema wanafahamu mbunge wao anachukiwa na baadhi ya watu ambao wanajihusisha na ufisadi kwani tangu alipochaguliwa amekuwa akipambana nao ili kutetea wananchi wanyonge.
Aidha, wananchi hao walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazozifanya za kuhamasisha uwekezaji nchini ambao umeanza kuleta manufaa makubwa kutokana na wawekezaji wengi kujitokeza kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwamo bandari.
Wananchi hao waliwapongeza wabunge walionyesha uzalendo kwa kupitisha azimio kuhusu pendekezo la kuridhiwa kwa mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwa lengo la kuanzisha ushirikiano katika uendelezaji wa maeneo ya bandari nchini.
Wabunge walipitisha azimio hilo jana Juni 10, 2023 siku ya Jumamosi baada ya kupata fursa ya kuchangia na kuishauri Serikali kuhusu mkataba huo.
Kabla ya wabunge kuchangia,Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Profesa Makame Mbarawa alipata nafasi ya kuuelezea mkataba huo na manufaa yake kwa Taifa na kufafanua hoja zilizoibuliwa na wadau ikiwamo ya muda wa utekelezaji wake.
Wananchi waliongeza kuwa nyota ya Musukuma ilianza kung’ara mwaka 2010 alipochaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Nzera,ambapo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita na alidumu kwenye nafasi hiyo kwa miezi nane baada ya kuwepo kwa madai ya madiwani kuhongwa na baadhi ya vigogo wa mgodi wa GGM ili wamuondoe kwenye nafasi hiyo maana alikuwa mwiba kwao.
Walisema wakati huo mafisadi hawakupumua kwani ,alikuwa anafanya ziara za kushitukiza mahospitalini usiku wa manane kuona kama wagonjwa wanatibiwa alifanya kazi kama alivyokuwa akifanya aliyekuwa Rais wa Tano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli na ndipo alipofanyiwa majungu na fitina na kung’olewa jambo lililoibua hasira kwa wananchi na kuandamana na wengine zaidi ya 1000 walihamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Mwaka 2013 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita na huko ndiyo aliwabana haswa mpaka walikoma,maana sasa alikuwa na nguvu kubwa hakuna ambaye angemuondoa na nafasi ambayo alidumu nayo mpaka mwaka 2015 alipochaguliwa kuwa Mbunge na kuwa na kofia mbili ambapo alilazimika kuacha nafasi moja baada ya kuwepo sheria ya kutokuwa na vyeo viwili.
Hata hivyo Mbunge Musukuma akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam alishangaa kuhusishwa na madai hayo akieleza kuwa gari hilo analodaiwa kununuliwa amelinunua kwa fedha zake na kulipa kodi ya Serikali na nyaraka zote za ununuzi anazo.
Mbunge Musukuma, akisisitiza jambo alipokuwa akichangia jambo Bungeni Dodoma.