Mhe. Balozi Luvanda (wa tatu kulia) akiwa na Bw. Shindo ( wa tatu kushoto) na wadau wengine wa Japan wakati wa zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania |
Wadau mbalimbali wa Japan wakishiriki hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa kahawa ya Tanzania kwenye migahawa ya Tully’s ya nchini Japan |
Balozi Luvanda akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya Tully’s nchini Japan, Bw. Daisuke Shindo |
Mhe. Balozi Luvanda akionesha baadhi ya kahawa za Tanzania zinazouzwa nchini Japan |
Kahawa ya Tanzania kama inavyoonekana pichani |
Kampuni ya Tully’s inayomiliki migahawa maarufu ya TULLY’s imezindua rasmi uuzaji wa kahawa ya Tanzania katika migahawa yao yote 700 iliyoko nchini Japan katika hafla iliyofanyika jijini Tokyo tarehe 9 Juni 2023.
Uzinduzi huo ambao ulienda sambamba na zoezi la uonjaji wa kahawa ya Tanzania, ulishuhudiwa na Balozi wa Tanzania
nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda; Mkurugenzi Mtendaji wa Mauzo wa Tully’s; Bw. Daisuke Shindo pamoja na Meneja Mkuu wa Idara ya Bidhaa za Vinywaji wa Kampuni ya Marubeni ambayo ni mbia wa Tully’s na miongoni mwa kampuni zinazosafirisha kwa wingi kahawa kutoka Tanzania kuingia nchini Japan, Bw. Masahiko Yoshimura.
Akitoa hotuba yake katika uzinduzi huo, Balozi Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na hata uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika
kilimo au sekta nyingine za Tanzania.
Aidha, amelitaja kuwa zao la
kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini ambalo linatumika kibiashara kwa
kulipatia Taifa pato kubwa kwa mauzo mengi ya kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan, kwa wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini Japan.
Balozi Luvanda alieleza kuwa, soko la kahawa nchini Japan bado ni kubwa, ikilinganishwa na matumizi na uhitaji wa Japan ambapo, Japan inahitaji wastani wa kilogramu milioni 453 (tani 453,000) za kahawa kwa mwaka na kutoa rai kwa watanzania hususan, wakulima wa zao la kahawa, watayarishaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wa zao hili kuchangamkia fursa ya soko kubwa la Japan ambalo linakua siku hadi siku.
“Napenda kutoa wito kwa watanzania wenzangu kuzingatia ubora wa viwango kwa mazao tunayolima nchini kwani nchi nyingi tunazouza bidhaa zetu hususan, hapa Japan wanazingatia
sana viwango.
Hivyo, ili kulikamata soko hili la Japan ipasavyo, inatupasa kwenda
sambamba na mahitaji ya kidunia ikiwemo, uzalishaji kwa viwango bora” alieleza Balozi Luvanda.
Vilevile, Balozi Luvanda alieleza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mifupi pamoja na maeneo ya msingi ya kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia
uhakika wa chakula, kulisha wengine kibiashara duniani, na pia wakulima kujipatia kipato cha kutosha ili kupunguza umaskini.
“Serikali ya Tanzania kwa kasi kubwa imewekeza kwenye rasilimali fedha na watu pamoja na uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza na kukifanya kilimo kuanza kutoa ajira zenye staha hususan, kwa vijana na wanawake, ikiwa ni pamoja na hatua ya kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo na kujenga msingi imara wa utekelezaji wa mipango ya kilimo yenye kutazama Tanzania ifikapo mwaka 2050”, alieleza.
Alihitimisha hotuba yake kwa kuelezea jitihada za ubalozi za kufanikisha azma ya Serikali ya
Tanzania katika mageuzi ya sekta ya kilimo ya kukifanya kuwa biashara.
“Ubalozi unatekeleza jukumu kubwa la kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini ikiwemo, mazao ya kilimo kama kahawa, kwa kuzitangaza bidhaa hizo na
kutafuta wawekezaji wa kuendeleza sekta mbalimbali kama vile sekta ya kilimo hususan, kilimo cha biashara kwa mazao ya kimkakati”, alihitimisha.
Kadhalika, Balozi Luvanda alihamasisha ushiriki wa
wadau wa kahawa nchini katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2023 (World Specialty Coffee Conference and Exhibition 2023) yatakayofanyika jijini Tokyo
kuanzia tarehe 27 hadi 29 Septemba 2023, ambayo yanaratibiwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania.
Tanzania ilishiriki kikamilifu katika Maonesho hayo kwa mwaka 2023 na manufaa yake yameonekana.
Tully’s Co. Ltd., inamiliki migahawa takribani 700 nchini Japan na imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa za aina mbalimbali duniani.
Kahawa ya Tanzania iliyozinduliwa ni kutoka Mashamba ya Kahawa ya GDM (GDM Farms) yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya.
Kuzinduliwa kwa kahawa ya GDM nchini Japan kunapandisha zaidi uhakika wa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na radha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee. Jina hili hutumika nchini Japan, kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Tanzania inasifika Japan kwa
kutoa kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini – full washed na
Arabica ngumu – natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera.
IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TAREHE 9 JUNI 2023