Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji, Juni9
Serikali imesitisha Shughuli za kilimo, katika vijiji vyote vilivyovamia eneo la misitu ya mikoko huko Maeneo ya Delta ya Rufiji Mkoani Pwani ili kuruhusu uendelevu wa hifadhi hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph kolombo Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa amefanya ziara ya kutoa maelekezo ya baraza la mawaziri baada ya kuazimia upembuzi yakinifu uliofanywa na jopo la mawaziri 8 katika maeneo hayo, na kubaini uwepo wa Shughuli za kibinadamu zinazokinzana na Uhifadhi wa Misitu ya mikoko na utunzaji wa mazingira.
Wananchi hao walitakiwa kusikiliza maelekezo yanayotolewa kwa umakini ili waweze kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Akisoma maelekezo hayo Kanali Kolombo alisema ,Moja ya maelekezo yaliyotolewa ni pamoja na kusitishwa kwa Shughuli zote za kilimo katika vijiji vilivyovamia eneo la misitu ya mikoko..
Vilevile Mkuu wa Mkoa alizielekeza Halmashauri na wakala wa Misitu Tanzania TFS kuanzisha kamati za vikundi vya Uhifadhi wa Misitu ya mikoko vitakavyojihusisha na utoaji wa elimu ili kuweza kudhibiti uoto wa asili uliopo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kupitia mikopo kufanya jitihada za kuiwezesha idara ya uvuvi kuunda vikundi ili wavuvi wapate zana za kisasa zitakazowasaidia kuvua katika maji ya kina kirefu.
Aidha Idara ya Mifugo na Uvuvi imeelekezwa kuandaa na kusimamia ratiba ya uvuvi wa kamba miti, kwa kuwashirikisha wadau wakiwemo wavuvi wadogo wadogo ambao kiuhalisia ndiyo Wahifadhi wakubwa wa eneo la misitu ya mikoko ambayo ndiyo chanzo cha mazalia ya samaki.
Awali Akisoma maazimio hayo,Mhandisi Felix Nlalio alieleza,baada ya Bunge kupokea mapendekezo ya uchunguzi uliofanywa limetoa maazimio manne ikiwemo kusitisha shughuli za kilimo katika vijiji vyote vya delta vilivyovamia eneo la misitu ya mikoko ili kuweza kuendeleza Uhifadhi huo.
Pia Kuanzisha kamati ya vikundi vitakavyokuwa vikitoa elimu ya Uhifadhi wa Misitu ya mikoko(VNR na BMU ) ,Wavuvi kuwezeshwa kupata zana zinazokubalika na kuweza kuvua katika maji ya kina kirefu, ili kuweza kupunguza nguvu kwenye maji ambayo ndiyo mazalia ya samaki.
Pamoja na hayo ratiba ya uvuvi wa kamba miti iandaliwe kwa kushirikisha Wadau ambao ni wavuvi wadogo wadogo .