OR TAMISEMI.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter M. Mtwale amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuwawezesha Maafisa Elimu Wilaya ili wazifikie shule zao kuona mazingira ya ufundishaji, ujifunzaji na kutatua changamoto zilizopo.
Mtwale ameagiza hayo leo tarehe Juni 7, 2023 wakati akifunga kikao kazi cha Maafisa Elimu wa Wilaya na Mikoa yote nchini kilicholenga kujadili na kutathmini utekelezaji wa Vigezo na Viashiria vya Utendaji Kazi (KPI) kilichofanyika Mkoani Tabora.
“Ili kubaini mafanikio na changamoto za ufundishaii na ujifunzaii, viongozi wa sekta ya elimu kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Kata hawana budi kutembelea shule zao, ambapo kupitia tathmini ya kikao kazi hiki nimejulishwa kuwa kasi ya utembeleaji wa shule inaridhisha” amesema Mtwale.
Mtwale ameagiza Maafisa Elimu kuongeza Usimamizi na Ufuatiliaji wa wanafunzi kumudu Stadi za Kusoma, Kuandika, Kuhesabu na lugha ya Kiingereza ambapo ameipongeza Mikoa iliyofanya vizuri katika kiashiria hicho ambayo ni ya Dar es salaam, Kilimanjaro, Njombe, Iringa na Arusha.
Aidha, Mtwale ameagiza kufanyika kwa vikao vya mara kwa mara vya tathmini ili kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi mapema ambapo licha ya kutathmini utendaji wa kazi vinatoa fursa ya kubadilishana uzoefu, ujuzi, maarifa na kudumisha mahusiano mazuri.
Amewataka Maafisa Elimu kuongeza kasi ya ufuatiliaji na usimamizi wa miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, nyumba za walimu, mabweni kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na ukarabati wa vituo vya walimu ambavyo vinaendelea kujengwa.
Kadhalika, Amewata Maafisa Elimu kuendelea kushirikiana na Walimu kutoa malezi bora kwa Wanafunzi ili kulinda desturi, mila na maadili ya Kitanzania ikiwa ni pamoja na kudumisha mahusiano mazuri mahali pa kazi ili kuepuka migogoro isiyokuwa na tija.