Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akipokea taarifa ya ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Isanjandugu iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya Juni 7, 2023. Katikati ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ilimbato Japhet, aliotoa taarifa hiyo na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota.
Na Dotto Mwaibale, Itigi
UONGOZI wa Wilaya ya Itigi mkoani Singida, umemlalamikia Diwani wa Kata ya Mitundu, Patrick Masanja kwa madai ya kukwamisha utekelezwaji wa miradi ya maendeleo katika kata hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Kemirembe Lwota alisema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba katika mfululizo wa ziara yake ya kukagua na kuhamasisha ukamilishaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali
wilayani humo Juni 7, 2023.
Kemirembe alisema kuwa diwani huyo Patrick Masanja amekuwa akiwazuia
wananchi kutokushiriki shughuli za maendeleo mbalimbali zinapofanyika katika kata hiyo.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa katika kata hii kikwazo kikubwa ni diwani wa
kata ya Mitundu kuwa na tabia ya kuwazuia wananchi wasishiriki kwa kutoa nguvu kazi wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendele,” alisema Kemirembe.
Aliongeza kuwa suala hilo wameliongelea katika vikao mbalimbali lakini bado diwani huyo anaendelea kuwakwamisha.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, John Mgalula akiomuongelea
diwani huyo mbele ya mkuu wa mkoa alisema hata walipokuwa wakitekeleza ujenzibwa kituo cha afya cha kata hiyo pia alikuwa akiwazuia wananchi kufanya kazi.
Afisa Tawala wa Wilaya hiyo, Laila Sawe alisema kabla ya diwani huyo
alikuwepo mtangulizi wake ambapo kazi za maendeleo zilikuwa zikifanyika bila ya vikwazo vya aina yoyote ambapo alimtaka Masanja abadilike.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Manyoni, Barnaba Mushi alisema chama hicho kinazifahamu vizuri changamoto na misuguano iliyopo baina ya diwani huyo dhidi ya viongozi wa wilaya hiyo na kuwa wanazifanyia kazi.
Diwani Patrick Masanja akijitetea mbele ya mkuu wa mkoa mara baada ya shutuma hizo kuelekezwa kwake alisema sio kweli kuwa yeye ana wazuia wananchi kutokushiriki kwenye miradi ya maendeleo, bali shutuma hizo zinatokana na chuki binafsi na hata baadhi ya viongozi wa
kata hiyo wanalielewa jambo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alimtaka diwani huyo abadilike kwani haiwezekani kila mtu amnyoshee kidole na kuwa jambo hilo halimjengi kisiasa.
Aidha Serukamba ameridhishwa na usimamizi mzuri na ukamilishwaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri hiyo na kuwapongeza viongozi wote kwa
ukamilishaji wa miradi hiyo kwa kiwango cha juu.
Pia Serukamba amewapongeza wataalam na wananchi kwa kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuchangia utalaam na nguvu kazi katika kutekeleza miradi hiyo ambayo imegharimu fedha nyingi.
“Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hii na jambo kubwa tunalopaswa kulifanya ni kuikamilisha kwa
thamani halisi ya fedha alizozitoa na kwa wakati uliopangwa,” alisema.
Miradi aliyoitembelea na kuikagua ni mradi wa ujenzi wa madarasa katika
Shule ya Msingi, Isanjandugu,, Kituo cha Afya Kata ya Mitundu, ujenzi wa
madarasa Shule ya Msingi Makale, ujenzi wa madarasa ya mikondo miwili Shule ya Msingi Mlowo ambao ujenzi wake utagharimu Sh. Milioni 493.4, ujenzi wa bweni labWasichana katika Shule ya Sekondari ya Mgandu, ujenzi wa Zahanati ya Kijijij cha Lulanga na Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Itigi inayojengwa eneo la Kitalaka.
Mhandisi wa Wilaya ya Itigi, Peter Shayo (kushoto) akielekeza jambo wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa hospitali hiyo.
|
Diwani wa Kata ya Mitundu, Patrick Masanja ambaye anadaiwa kuzuia wananchi wasitekeleze miradi ya maendeleo. |