Na Kassim Nyaki, Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake imeweka kambi katika viwanja vya bunge jijini Dodoma kwa ajili ya kutoa elimu ya shughuli za uhifadhi na kunadi vivutio vya utalii vinavyopatikana hapa nchini.
Taasisi za Wizara hiyo zinazoshiriki maonesho hayo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Akiwa katika ziara ya kutembelea maonesho hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) ameeleza kuwa wabunge ni wadau muhimu katika shughuli za uhifadhi na utalii ndiyo maana katika kipindi cha Bunge la bajeti wizara imeamua kuwafikia waheshimiwa wabunge na kuwaongezea uelewa wa mazao ya utalii na shughuli za uhifadhi zinazofanyika ili waendelee kuwa mabalozi katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
“Wakati ni sasa, tuna kila kitu katika nchi yetu lazima tuhakikishe tunatangaza maeneo yote ya vivutio vya utalii kwa ubunifu wa hali ya juu na maeneo ya kipekee kama nyayo za Laetoli, vituo vya malikale na kuibua mazao mapya ya utalii na kuyatangaza kwa nguvu ili yaongeze idadi ya watalii na mapato kwa nchi yetu kwa zaidi ya asilimia 100 ya tulivyo sasa” ameongeza Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa amewapongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuja na zao jipya la utalii wa anga kupitia kimondo cha Mbozi ambacho kwa sasa uhifadhi na utalii katika eneo la Kimondo hicho umeimarishwa kwa kuongezewa makumbusho yenye kumbukumbu na historia za tamaduni zetu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NCAA, Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amepongeza juhudi za Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake kutangaza vivutio vya Utalii kwa Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi na sauti zao zinasikika kuelezea jambo kwa uhalisia wake.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Elibariki Bajuta ameeleza NCAA itaendelea kutekeleza mikakati ya Wizara kwenye kutangaza utalii ili kuongeza idadi kubwa ya wageni kutembelea maeneo ya hifadhi za wanyamapori, urithi wa utamaduni na mambo kale.
Ameeleza kuwa tarehe 30 Juni, 2023 NCAA inatarajia kuadhimisha siku ya kimondo duniani ambapo maadhimisho hayo yataenda sambamba na kufanya warsha na kongamano la kisayansi elimu ya anga, mashindano ya riadha, maonesho ya vivutio mbalimbali vilivyoko kusini mwa Tanzania na kutoa elimu na Utalii wa anga.