NA MWANDISHI
WETU, MWANZA
ASILIMIA 87 ya
shughuli zote za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) zinafanyika kwa njia ya
Mtandao. Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa
Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar amewaambia Maafisa Utumishi/Utawala, Afya na
Usalama kutoka Taasisi za Umma na Binafsi kwenye kikao cha
kujenga uelewa wa huduma zinazotolewa na WCF na namna zolivyoboreshwa
kwa matumizi ya wanachama.
Akiongea kwenye mafunzo kwa maafisa Rasilimali Watu, Utawala na Usalama
na Afya mahali Pa kazi kutoka taasisi za Binafsi na Umma, jijini
Mwanza, Dkt. Omar alisema kutokana na matumizi
hayo ya teknolojia ya kisasa katika kuwahudumia wadau, afisa wa WCF anaweza
kuingia kwenye mtandao na kutoa huduma yoyote ya Mfuko wakati wowote na mahli
popote pale ilimradi kuna mtandao (mawasiliano ya internet).
Wakati wa ufunguzi Dkt. Omar amesema
“Dhumuni kubwa la mafunzo haya ni kuwapa uelewa kuhusu huduma zitolewazo na WCF, hatua
za kufuata wakati wa kuwasilisha madai hususan kuwasilisha madai kwa njia ya
mtandao (Online Notification System-ONS) inayopatikana kwenye portal.wcf.go.tz
na masuala ya Usalama na Afya mahali pa
kazi” Alifafanua
Katika kikao hicho, maeneo makubwa matatu yaliyojadiliwa ni pamoja na kukuza uelewa wa namna ya
kudhibiti ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Dr. Omar ameongeza kuwa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu
ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha
Tanzania ina uchumi endelevu na kuwakwamua wananchi kutokana na umasikini kwa
kutoa fursa mbalimbali za uwekezaji nchini.
Amesema
ili kuendana na dhamira hiyo nzuri wadau wote kwa namna moja ama nyingine hawana budi kuongeza ubora wa bidhaa na huduma bali vilevile kuboresha
mazingira ya uzalishaji ili kuepuka au kuzuia changamoto
mbalimbali za ajali na magonjwa mahali pa kazi.
“Hivyo basi
dhamira hii itawezekana pale ambapo tutakuwa na wafanyakazi wenye uhakika wa
usalama wa afya zao katika maeneo yao ya kazi na endapo itatokea bahati mbaya
wakapata madhara wakiwa wanafanya kazi basi wawe na kinga ya kipato na hata
ikitokea mfanyakazi amefariki basi wategemezi wake waweze kupata fidia stahiki
na kwa wakati.” Alisema.
Alisema ndio
maana WCF itaendelea kutoa elimu hiyo kwa maafisa hao kutokana na umuhimu wao
katika utoaji wa taarifa zinazohusiana na fidia kwa wafanyakazi pindi
wanapokumbwa na changamoto za ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.
“Ni jambo jema kuona wadau kutoka maeneo tofauti tofauti hususan
maeneo ya migodi na ninafahamu juhudi kubwa ambazo zinafanyika huko katika
kulinda afya na usalama wa wafanyakazi na pia ninafahamu wapo wanaotoka katika
taasisi za umma wanaosimamia rasilimali watu, wote hawa tungependa wajue mambo ya msingi katika kudhibiti ajali na magonwja yatokanayo
na kazi.” Alifafanua.
Aidha
aliwakumbusha Maafisa Rasilimali Watu/Utumishi kujenga mahusiano mazuri baina
ya ofisi zao na wafanyakazi katika kulinda haki zao ikiwa ni pamoja na kufahamu
masuala yahusuyo fidia baada ya mfanyakazi kuumia, kuugua ama kufariki kutokana
na kazi.
Amesema awali mafunzo kama hayo yaliwahusisha Maafisa Rasilimali watu pekee “Hata
hivyo tuliona ni muhimu kundi la Maafisa Usalama Mahali pa Kazi wakiungana na Maafisa Utumishi/ Utawala kwa
pamoja waweze
kupata elimu hii ili wajue namna ya kudhibiti ajali na magonjwa yatokanayo na
kazi na jinsi ya kuwasilisha taarifa pindi matukio hayo ya ajali au ugonjwa yapotokea
ili kuwasilisha taarifa kwenye Mfuko kwa wakati na
hii itawezesha wafanyakazi kupata haki zao za
msingi.” Amefafanua.
Ninyi ni daraja
muhimu kati ya WCF na wafanyakazi wote wanaopata
changamoto. Wewe ukiweza kujua taratibu
zinazohitajika kuwasilisha madai WCF utasaidia
kwa kiasi kikubwa hawa wafanyakazi kuweza kupata stahiki zao, alisema Dkt.
Omar.
Aidha mmoja wa
washiriki Bi. Izmina Ally Meneja wa Afya na Usalama kazini kampuni ya SBC,
alisema amefurahishwa na jinsi WCF ilivyotoka
kwenye matumizi ya analojia na kwenda kidigitali katika kuwasilisha madai ya
wafanyakazi wanaoumia au kuugua kazini
“Hii
itaturahishia sana katika kuwasilisha taarifa pindi panapotokea matukio hayo kwa mfanyakazi na
itaondoa lawama ya kuchelewa kutoa taarifa na
hili nitalifikisha kwenye utawala na wafanyakazi wote
wajue.” amesema.
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar, akizungumza na washiriki Juni 5, 2023
Baadhi ya washiriki
Baadhi ya washiriki