Waendesha Pikipiki wakipita kwa tabu kwenye daraja la miti katika mto Kotoko kaya ya Rwinga wilayani Namtumbo.
Sehemu ya barabara inayounganisha kijiji cha Matepwende na kitongoji cha Zanzibar wilayani Namtumbo ikiwa imeharibika vibaya na mvua za masika na hivyo kuhitaji kufanyiwa matengenezo makubwa ili kurahisisha shughuli za usafi na usafirishaji wa mazao.
Baadhi ya mafundi wakianza ujenzi wa daraja katika mto Kotoko kata ya Rwinga wilayani Namtumbo ambapo litakapo kamilika litawezesha kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi wa kitongoji cha Zanzibar na Namtumbo mjini.
………………….
Picha na Muhidin Amri,
KILIO cha muda mrefu cha wakazi wa kijiji cha Matepwende na kitongoji za Zanzibar wilayani Namtumbo, kukosa mawasiliano ya uhakika kutokana na mto Kotoka unaotenganisha maeneo hayo kujaa maji kimepata majibu baada ya Wakala wa barabara za mijini na vijijini(Tarura)kuanza ujenzi wa daraja la kisasa katika eneo hilo.
Mradi huo umetengewa jumla ya Sh.milioni 638 ambazo zitatumika kujenga daraja lenye urefu wa mita tano,makalavati matatu na kazi ya kufungua barabara mpya yenye urefu wa kilomita 34 kazi inayotarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu.
Mtimba alisema,mradi huo unalenga kurahisisha mawasiliano na shughuli za usafiri na usafirishaji wa bidhaa ikiwemo mazao kutoka shambani kwenda sokoni na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Alisema,kwa sasa wananchi hasa wakulima wanapata shida kubwa kupita katika mto huo kutokana na ubovu wa barabara,lakini ujenzi wa daraja utakapokamilika changamoto hizo zitamalizika na hata kupungua kwa gharama za usafirishaji wa bidhaa na mazao.
Aidha alisema,ujenzi wa daraja na ufunguzi wa barabara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Tarura kufungua barabara hadi kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa na kufika kusiko fikika ambapo Tarura imejipanga kuendelea kufungua barabara mpya katika maeneo mbalimbali wilayani Namtumbo.
Amewaomba wananchi,kuhakikisha wanatunza daraja hilo ili liweze kudumu kwa muda mrefu na kuepuka kufanya vitendo vinavyoweza kuchelewa kukamilika kwa mradi huo mkubwa unaotekelezwa kwa faida yao.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Matepwende,wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kujenga daraja katika mto huo ambao kwa muda mrefu umekuwa sehemu ya kukithiri kwa umaskini kwenye familia zao.
Abbas Yasin ameiomba serikali kupitia Tarura,kuharakisha ujenzi wa daraja na ufunguzi wa barabara hiyo ili waweze kuitumia kusafirisha mazao hasa msimu huu wa mavuno ulianza tangu mwezi Mei.
Alisema,barabara hiyo ni kero kubwa na ndiyo iliyosababisha wao kuwa na kiwango kikubwa cha umaskini kwani licha ya kuzalisha kwa wingi mazao ya chakula na biashara,lakini wameshindwa kupiga hatua na kunufaika na kazi za kilimo kwa sababu ya kushindwa kusafirisha mazao yao hadi sokoni kutokana na ubovu na kupanda kwa gharama za usafirishaji.
Alieleza kuwa,kutokana na hali hiyo wafanyabiashara wasiokuwa na huruma wanatumia nafasi ya kwenda moja kwa moja mashambani na kununua mazao kwa bei ndogo isiyolingana na uzalishaji mashambani.
Mkulima wa kitongoji cha Zanzibar Yakin Kanyalo alisema,kukosekana kwa daraja katika mto Kotoko na ubovu wa barabara hiyo unasababisha wanawake wajawazito,wazee na watoto kushindwa kufika kwa wakati kwenye vituo vya afya.
Aliongeza kuwa,wapo wananchi waliopoteza maisha kwa kushindwa kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pindi wanapopatwa na ugonjwa wa ghafla,mama wajawazito kujifungulia njiani wakati wakipelekwa kupata huduma kituo cha Afya Namtumbo au Hospitali ya wilaya.