MKOA Wa Dar es Salaam umetangaza kujikita kwenye kampeni ya kuongeza uelewa kwa wanachi juu ya umuhimu wa Bima ya afya iliyoboreshwa na kujiunga nayo ili waweze kupata huduma bora za matibabu kwa urahisi.
Hayo yalibainishwa jana Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Bima ya Afya iliyoboreshwa i-ICHF Mkoa wa Dar es Salaam, Yasin Kisawike alipozungumza na waaandishi wa habari kando mwa mkutano baina ya Maafisa Rasilimali Watu na wawakilishi wa wafanyakazi.
Alisema bima hiyo iliyoboreshwa ni muhimu kwa matibabu ya familia na kupunguza gharama kubwa za matibabu ambazo mara nyingi zinakuja gjafla.
Kisawike alisema kuwa pamoja na umuhimu wake, ni watu wachache kwenye jamii wamejiunga na bima hiyo ya matibabu.
Aliongeza kusema kuwa kwa sasa ni asilimia 11 tu ya wakazi wa jiji wamejiunga na bima hiyo ya afya kati ya watu million 5 na ni asilimia 15 tu ya Watanzania wote wamejiunga na Bima mbalimbali ikiwemo iliyoboreshwa na Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya(NHIF) NHIF.
“Leo tumewaalika maafisa rasilimali watu na wawakilishi wa wafanyakazi kujadili u,uhimu wa kujiunga na bima hii kwa ajili ya afya zao,”alisema Kisawile akiongeza kuwa “Lengo la kampeni yetu ni kutoa elimu kwa jamii ili wajunge na huu mfuko wa bima ya afya iliyoboreshwa ili wapate uhakika wa huduma za afya,”.
Naye Mwakilishi wa Wafanyakazi kutoka Kampuni ya TLL Printing and Packaging Joseph Mabaga aliwaomba wafanyakazi nchini kujiunga na bima ya afya.
Mabaga alisema kuwa bila ya kuwa kuwa na wafanyakazi wenye afya nzuri, uzalishaji wa tija kwenye viwanda vyetu hautaweza kufikiwa.
Bima ya Afya iliyoboreshwa ilianzishwa kama bima ya jamii(CHF) mwaka 1990 na baadaye iliboreshwa na kuzinduliwa mwaka 2014.