Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Godfrey Daniel Chongolo amehitimisha ziara yake ya siku saba (7) Mkoa wa Iringa, baada ya kutembelea majimbo yote na halmashauri zote ambapo kupitia ziara hiyo, Chama kimeendelea kusisitiza umuhimu wa Viongozi wa Chama na Serikali katika ngazi mbalimbali, hususan kuanzia mikoa hadi kitongoji, kuendelea kushuka chini kwa wananchi, kuwasikiliza kwa ajili ya kuzibaini changamoto zao na kuzitatua.
Aidha, kupitia ziara hiyo iliyokuwa na malengo makuu matatu; kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025, kukagua na kuhamasisha uhai wa chama na kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi, ambayo ni mwendelezo wa ziara za namna hiyo ambazo Katibu Mkuu amekuwa akizifanya katika maeneo mbalimbali nchini, Chama kimeendelea kusisitiza viongozi na watendaji waliopewa dhamana mbalimbali za umma, kuwatumikia wananchi wakati wote.
Pamoja na kuwapongeza viongozi na watumishi waliopewa dhamana ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, kwa jinsi wanavyoendelea kutekeleza wajibu wao wa kutafuta majawabu ya changamoto za wananchi, Chama Cha Mapinduzi kinawaelekeza wahusika hao, hasa kupitia kwa Makamisaa wa Chama wa Mikoa na Wilaya, kote ambako Chama kitaendelea kufanya ziara zake, kujipanga kutoa ufafanuzi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hasa inavyozingatia thamani ya fedha na kutatua changamoto za wananchi, kwa kadri ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekusudia muda wote.
Kupitia ziara hizo, Chama pia kimeendelea kuwaelekeza Viongozi na Watendaji wote kuwa Chama Cha Mapinduzi, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kinatarajia watatumia dhamana zao kuleta ufanisi na kuleta matokeo yanayotarajiwa na Watanzania katika maeneo yao na kuwa CCM haitamvumilia kiongozi au mtendaji yeyote anayekwamisha utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa wananchi.
Aidha, pamoja na masuala mengine Katibu Mkuu Ndugu Chongolo, katika ziara yake aliyoihitimisha mkoani Iringa, amesikiliza na kupokea changamoto mbalimbali za jumla na mahsusi katika sekta za barabara, elimu, afya, maji, kilimo, umeme, umwagiliaji na kuzitoa maagizo kwa mawaziri wa sekta husika, makamisaa wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanafika kwa wananchi wa maeneo hayo na kutatua kero hizo.
Chama Cha Mapinduzi kinatoa shukrani za dhati kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa kwa mapokezi, ushirikiano, upendo, mwitikio wao wakati wa ziara hiyo, Katibu Mkuu tangu alivyofika mkoani humo tarehe 26, Mei, 2023 hadi tarehe 2 Juni, 2023, ambayo pia waliitumia kutuma salaam zao za kumshukuru na kumuunga mkono Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake makini na mahiri katika kuwatumikia Watanzania. Chama kinawaahidi kuwa kitafuatilia kwa karibu maelekezo yote yaliyotolewa kwa watendaji wa serikali kwa ngazi zote, kwa ajili ya kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi inaendelea kutafsiriwa kwa vitendo kwa ajili ya manufaa na maslahi ya taifa letu na Watanzania wote kwa ujumla.