MAZINGIRA ya elimu yanafaa kuboreshwa na kuwa na miundombinu rafiki ,kuanzia Ngazi ya awali ili kufikia safari ya elimu ya msingi hadi ngazi za vyuo vikuu.
Hatua hii ni njema kwakuwa mafanikio ya watu wengi katika Taifa lolote msingi wake ni shule za awali kwani huwezi ukaanza elimu ya juu pasipo kupitia shule za awali, pre schools ili kujijenga kiufahamu.
“Tunaishukuru Serikali yetu kuliona hili na Sasa tunashuhudia juhudi za kuboresha sekta ya elimu zikipenyezwa kuanzia madarasa ya awali ,vituo vya Utayari kama ilivyokuwa nguvu zikipelekwa kwenye shule za Msingi, Sekondari na Vyuo.
Ofisa elimu Mkoani Pwani,Sara Mlaki anaeleza namna mradi wa Shule bora ulivyoleta Mapinduzi na Mageuzi Makubwa ,katika kuanzishwa vituo vya Utayari 38 mkoani hapo, ili kusogeza elimu kwa watoto wa miaka 6-9 ambao walikata tamaa ya kukosa elimu ya awali ili kuanza elimu ya Msingi.
Alieleza, lengo la vituo vya Utayari ni kusogeza huduma ya kielimu karibu, na kuondoa wimbi la watoto majumbani wakiwemo watoto wa wafugaji ambao walishindwa kujiunga na shule za awali ili kujiandaa na elimu ya Msingi.
“Wazazi wengi wameonyesha mwamko kutoa watoto wao ,na watoto hawa wananolewa ili kuanza darasa la kwanza ambapo mbinu mbalimbali za kufundishishia zinatumika kuwapa uelewa ikiwemo hadithi,nyimbo na michezo”
Matokeo hadi sasa zaidi ya watoto 1,422 katika vituo 38 vilivyoanzishwa watapata fursa ya kujiunga na darasa la kwanza na hatua hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kujua Kusoma Kuandika na Kuhesabu(KKK).
Sara anasema, hii imesaidia kupunguza watoto kufuata elimu umbali mrefu na Idadi ya watoto wanaopata elimu ya awali kuongezeka na idadi ya wanafunzi kujiunga darasa la kwanza kuongezeka na idadi ya wanafunzi wasiomudu KKK wanapoanza darasa la kwanza kupungua sana.
Hata hivyo, alifafanua kuna vituo vya Utayari vinne kila Halmashauri Mkoani humo katika kata mbili, ambako Bagamoyo vipo kwenye kata ya Makurunge,Fukayose.
Vingine vipo Chalinze katika kata ya Lugoba na Ubena Zomozi, Halmashauri ya Kisarawe kwenye kata ya Masaki na Msimbu, Halmashauri ya Kibaha Mjini Mkuza na Visiga, Halmashauri ya Kibaha Vijijini Mtambani,Ruvu Station, Halmashauri ya Mafia katika kata ya Baleni,Kilindoni, Halmashauri ya Rufiji -Umwe na Ngolongo, Kibiti -Mjawa na Kiongoloni.
Vilevile Sara alisema ,elimu ni pamoja na watoto wa makundi yote,hivyo aliwaomba wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu wasiwafiche na badala yake watumie fursa ya uwepo wa vituo hivyo kujiandaa na elimu ya msingi.
Alisema watoto hao nao wanahitaji maandalizi ya elimu kama ilivyo kwa wengine ili kuanza safari yao ya kitaaluma na sio kuwafungia majumbani.
CHALINZE
Ofisa Elimu Awali na Msingi Chalinze Miriam Kihiyo, anaeleza, vituo vya Utayari wanavyo vinne katika kata ya Lugoba na Ubena Zomozi.
“Tulihamasisha jamii kujenga vituo, pia madiwani na walipewa semina Kuhusiana na vituo hivi,na watoto wanapata mafunzo kupitia njia na mbinu mbalimbali za Ufundishaji ikiwemo hadithi, michezo,wanapewa pia uji wakiwa shuleni.”
Kihiyo alieleza kuwa, lengo la vituo hivyo Kutoa fursa ya kusoma elimu ya awali kwa watoto wanaoshindwa kujiunga na shule kutokana na uwepo wa mazingira hatarishi (mfano; misitu, wanyama, mito, kuvuka barabara kubwa, n.k) kati ya nyumbani na shuleni ikiwemo umbali mrefu wa kuifikia shule.
“Kuna eneo la Mkese huko watoto wa wafugaji ni wengi walikuwa hawajui hata kiswahili kabisa, walikuwa hawajui Kusoma Kuandika wala Kuhesabu lakini kwasasa wengi wao wamejiunga na vituo vya Utayari,wamepata mwalimu ambae ni mmasai mwenzao anawafundisha na wanajua hata kuongea kiswahili”
‘”Wahanga katika hili la kukosa elimu ya awali na kukosa fursa ya kielimu ipo sana kwa Hawa wenzetu wafugaji,lakini Tunashukuru wameanza Kuwa na mwamko, watoto tumewakusanya eneo moja na kupatiwa elimu”anaeleza Kihiyo.
Kihiyo alieleza, mafanikio kwa sasa watoto wanapenda kwenda shule kuliko kubaki nyumbani kufanya kazi za kilimo, kufuga na hivyo, kupunguza utoro.
Katika hatua nyingine, alitaka changamoto ni Upatikanaji wa Miundombinu Bora ya kujifunzia kwenye maeneo ya karibu na makazi na upatikanaji wa Walimu Wenyeji wenye sifa za kufundisha watoto.
Wakati huo huo, Kihiyo alieleza wanaendelea kukabiliana na changamoto ya wazazi kuwa na mwamko wa elimu ya watoto wao kwani ndio changamoto kubwa.
MKURANGA
Ofisa Elimu Awali na Msingi Halmashauri ya Mkuranga Jessy Mpangala anashukuru serikali na mkoa kwa kuwa na mpango huo ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya watoto majumbani ambao walikosa fursa ya Shule za awali karibu na maeneo wanayoishi.
Alieleza, Mkuranga vipo vituo vya Utayari sita katika kata ya Vianzi,Delta na Nyamato.
Maofisa Elimu Kata ya Njianne Bakar Jiri na ofisa Elimu Kata ya Magawa Azania Kimeru walieleza mradi wa shule bora umeleta mafanikio makubwa ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji.
Walieleza, watoto wanapelekwa kupata elimu ya awali na kutumia vituo vya Utayari ili kuandaliwa kujiunga na darasa la kwanza.
MALENGO, KAZI,UTEKELEZAJI WA MRADI KITAIFA
Mradi wa Shule Bora umelenga kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuinua kiwango cha elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wote wa kike na wa kiume katika shule za Serikali za Tanzania.
Kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania mradi huu utafanya maboresho yatakayowezesha kila mtoto kupata msingi mzuri katika elimu yake ya awali, ili kuitumia fursa kwa kutoa mchango wake katika ukuaji wa nchi na maendeleo yake.
Tarehe 4 april mwaka 2022,” Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza ilizindua mpango wa elimu bunifu wa shule bora wenye thamani ya Sh.Biln271 ,utakaosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia, ujumuishi na usalama kwa wasichana na wavulana katika shule za msingi nchini.
Mradi huo ,unatekelezwa kwa msaada wa Serikali ya watu wa Uingereza “UKaid” wakishirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) ,katika mikoa Tisa ya Tanzania Bara ikiwemo Pwani, Tanga,Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi, Simiyu, Mara na Rukwa.