Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Salome leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Salome Makamba kuhusu mkakati wa Serikali wa kutengeneza mazingira rafiki kwa taasisi za kifedha kuwapa mikopo wachimbaji wadogo kwa kuzingatia mazingira yao ya upatikanaji na uzalishaji wa madini.
Na Lilian Lundo – MAELEZO.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko kufuatilia taasisi za fedha zinazowakopesha wachimbaji wadogo na kuhakikisha wanawakopesha wajasiriamali hao kwa riba ndogo ili wafanye kazi hiyo kwa faida.
Waziri Mkuu amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Salome Makamba kuhusu mkakati wa Serikali wa kutengeneza mazingira rafiki kwa taasisi za kifedha kuwapa mikopo wachimbaji wadogo kwa kuzingatia mazingira yao ya upatikanaji na uzalishaji wa madini.
“Tunatambua ipo changamoto na masharti mbalimbali ya taasisi za fedha, tulichofanya ni kutoa maelekezo kwa taasisi hizo, kwanza kujua mtu anayekopa anataka kufanya shughuli gani, pia kujua muda wa shughuli husika kuanzia uwekezaji wake mpaka uzalishaji wake, ili masharti yalenge utendaji wa sekta hiyo. Kwa sababu kila eneo lina muda wake wa uwekezaji na uzalishaji wake wa kuingia kwenye masoko,” alisema Mhe. Waziri Mkuu.
Aliendelea kwa kusema kuwa, haitakuwa vizuri kama mchimbaji mdogo ambaye anachimba madini hadi kuuza ndani ya miezi sita, lakini anapewa mkopo wa miezi mitatu.
Aliongeza kuwa mara kadhaa wamehamasisha taasisi za fedha kufanya tafiti za uchimbaji mdogo na kuwafikia wachimbaji wadogo sambamba na kuwakopesha kwa riba nafuu na ikiwezekana bila riba ili kuwawezesha vijana ambao ni wajasiriamali kupata mikopo na kuitumia ili wapate faida.
“Serikali inaendelea kukaa na taasisi za fedha kuzihamasisha kutenga mitaji kwenye dirisha hilo kwa masharti lakini waangalie utendaji wa sekta hiyo, ili wajasiriamali waweze kupata mikopo yao vizuri na pia tumewataka wajasiriamali hao kuunda vikundi kwani wakiwa kwenye vikundi ni rahisi zaidi, kwa sababu taasisi nyingi zinaogopa kupoteza fedha, kwa hiyo ushirika ni mkombozi,” alisisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Aidha amesema kuwa, kwa upande wa Serikali, halmashauri zina mikopo midogo kwa vijana, wanawake na walemavu, pia kuna mifuko ya uwezeshaji ambayo maeneo yote hayo ni fursa kwa vijana kupata mikopo.