Mhe. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza hayo leo Juni 1, 2023 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mvumu, Mhe. Livingstone Lusinde kuhusu mpango wa Serikali wa kuwapeleka wataalam katika vituo vya afya vilivyojengwa na Serikali nchi nzima, ambavyo asilimia kubwa ya vituo hivyo vina upungufu mkubwa wa wataalam wa afya
….
Na Lilian Lundo – MAELEZO .
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa vibali kwa Wizara ya Afya na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuajiri watumishi wa sekta ya afya ili kuwapeleka katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zote nchini ili waweze kutoa huduma.
Mhe. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza hayo leo Juni 1, 2023 bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mvumu, Mhe. Livingstone Lusinde kuhusu mpango wa Serikali wa kuwapeleka wataalam katika vituo vya afya vilivyojengwa na Serikali nchi nzima, ambavyo asilimia kubwa ya vituo hivyo vina upungufu mkubwa wa wataalam wa afya.
“Serikali yetu tangu Awamu ya Tano na sasa ya Sita, imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa maeneo ya kutolea huduma nchini, kama vile zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri, za wilaya lakini pia za mikoa na kanda, na sasa tunaimarisha huduma kwenye hospitali za kitaifa,” alisema Mhe. Waziri Mkuu.
Aliendelea kusema kuwa, awamu ya kwanza ilikuwa ujenzi wa miundombinu, ambayo ni majengo na kazi hiyo imefanyika vizuri.
Awamu ya pili ni kupeleka vifaa tiba na madawa, ambayo sasa inaendelea.
“Katika eneo la watumishi, kazi inaendelea ambapo Rais wetu ameshatoa vibali kwa Wizara ya Afya pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuajiri watumishi wa sekta ya afya ili kuwapeleka maeneo yote ya zahanati, vituo vya afya na hospitali zote nchini,” alisisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Aliendelea kwa kusema kuwa, Serikali inatambua mahitaji ya wataalam wa sekta ya afya ni mkubwa, hivyo Serikali itaendelea kuajiri kulingana na uwezo wa kifedha kwa lengo la kutoa huduma kwa Watanzania kwenye maeneo yao. Aidha, aliongeza kuwa Serikali inafanya mapitio, kutokana na baadhi ya maeneo hasa mijini kuwa na watumishi wengi kuliko vijijini.
Hivyo itawahamisha baadhi ya watumishi katika maeneo ambayo wamelundika na kuwapeleka kwenye uhitaji.
“Nitoe maelekezo kwa Wakurugenzi kufanya mapitio ya kina ya idadi ya watumishi tulionao na maeneo yenye mrundikano mkubwa kuwahamisha na kuwapeleka kwenye maeneo ambayo yana watumishi wachache. Lengo la Serikali ni huduma hizi zitolewe kwa usawa katika maeneo yote nchini,” alibainisha Mhe. Waziri Mkuu.