Na Hellen Mtereko, Mwanza
Shirika la Americares limekabidhi vifaa tiba vya kutibu ugonjwa wa fistula ya uzazi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando iliyoko Jijini Mwanza vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 200 kwa lengo la kuendelea kuimarisha huduma kwa wagonjwa.
Hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo imefanyika leo Alhamisi Juni 1, 2023 katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.
Dkt.Nguke Mwakatundu ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Americares amesema kinamama 2500 hadi 3000 wanapata tatizo la fistula ya uzazi nchini kati ya hao wanaopata matibabu ni 2000 hali inayoonyesha tatizo hilo ni kubwa na inapaswa kuongeza jitihada za kuutokomeza kabisa.
Dkt. Mwakatundu ameeleza kuwa kwakutambua mchango mkubwa unaotolewa na Hospital ya Rufaa ya Kanda Bugando katika juhudi za kutokomeza tatizo hili tuliona ni vyema kununua vifaa vya upasuaji na vifaa tiba ili kuwawezesha kuendelea kutoa huduma za fistula kwa kiwango chenye ubora wa juu.
“Baadhi ya vifaa vya upasuaji tulivyo nunua ni Mashine ya kutolea dawa za usingizi kwenye upasuaji,kitanda maalumu cha kisasa cha upasuaji pamoja na taa ya kumulikia wakati wa kufanya upasuaji”, amesema Dkt.Mwakatundu.
Amesema pamoja na kutoa vifaa hivyo wataendelea kushirikiana na Serikali pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando katika kutoa huduma za fistula na kushiriki kikamilifu kutokomeza ugonjwa huo.
“Tunaiomba Serikali iendelee kuliangalia kwa makini tatizo la fistula ili matibabu yake yapatikane kwa urahisi nchini hatua itakayosaidia wagonjwa kupata huduma hiyo katika maeneo yao”, amesema Dkt.Mwakatundu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt.Fabiani Masaga amesema ugonjwa wa fistula humpata mwanamke mjamzito ambae hupata uchungu pingamizi wa muda mrefu unaotengeneza tundu lisilo la kawaida kati ya njia ya uke na kibofu cha mkojo au njia ya haja kubwa.
“mwanamke mwenye tatizo hilo hutokwa haja ndogo na kubwa kupitia njia ya uzazi mfululizo bila kutambua jambo ambalo humkosesha raha na kumsababishia adha zitokanazo na kulowa kila wakati,harufu mbaya,kutengwa na jamii,kuporomoka kiuchumi pamoja na msongo wa mawazo”, amesema Dkt.Masaga
Amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando inapokea wagonjwa wa fistula zaidi ya 300 kwa mwaka na miongoni mwao hufanyiwa upasuaji na wengine hufanyiwa huduma ya viungo tiba.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amewaomba wasimamizi wa Hospital hiyo kutunza vifaa tiba hivyo ili viweze kufanya kazi iliyokusudiwa ya upasuaji kwa wagonjwa wa fistula.