Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni Bi. Elizabeth Mokiwa akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 1/6/2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji wa kipindi cha kuanzia January hadi March 2023
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufatilia miradi ya maendeleo miwili yenye thamani ya Sh. 3, 941, 157, 212 huku mradi wa ujenzi wa madara 12 ya Shule ya Sekondari Godwin Gondwe uliopo Kunduchi ukiwa na dosari ya thamani ya fedha na kiwango cha ujenzi haviendani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 1 /6/2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa ripoti ya utendaji wa kipindi Cha kuanzia January hadi Machi 2023, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bi. Elizabeth Mokiwa, amesema kuwa mradi mwengine ni ujenzi wa jengo la Utawala la Manispaa ya Kinondoni ambapo ujenzi wake umechelewa kukamilika hivyo TAKUKURU imeanza kuchuguza miradi hiyo.
Bi. Mokiwa, amesema kuwa wanaendelea na ufatiliaji ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia muda wa mkataba unavyoeleza.
Hata hivyo amesema utekelezaji wa programu ya TAKUKURU – Rafiki unaendelea na kufanikiwa kufika katika Kata tano katika Manispaa ya Kinondoni.
Amesema kuwa wamepokea taarifa 35 zilizohusu rushwa, huku akieleza kuwa malalamiko mengi yalihusu madai, dhuluma, kughushi, kutapeli, mikopo umiza pamoja na kutoridhishwa na kesi Mahakamani.
“Malalamiko haya ni yale yanayohusu tuhuma zilizopo katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA) pamoja na Sheria nyinginezo” amesema Bi. Mokiwa.
Amebainisha kuwa mahakamani wamefanikiwa kushinda kesi mbili kuhusu rushwa na mpaka sasa kuna mashauri 22 yanaendelea Mahakamani.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa mikakati yao ni kuhakikisha TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni inatoa huduma inayowafikia wananchi wote na inaendelea na utekelezaji wa programu ya TAKUKURU – Rafiki kwa kuendeleza ushirikiano na wananchi.
“TAKUKURU – Rafiki nimepewa ushirikiano na viongozi pamoja na watoa huduma ambao wamekuwa na utayari kwenye kushiriki na utatuzi wa kero zinazoibuliwa kwenye vikao” amesema Bi. Mokiwa.
Amefafanua kuwa ili kuhakikisha jamii inakuwa na uwelewa mpana kuhusu rushwa wameendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia njia ya semina, mkutano ya hadhara pamoja na kutumia klabu za rushwa katika Shule za Sekondari na Msingi.
“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU pamoja na kuepuka matapeli wanaibuka na kuwapigia simu wananchi kwa kujifanya wao ni Maafisa wa TAKUKURU, huku wakiwatapele watu kwa kuwatisha kuwa wana tuhuma zao na kuwadai pesa ili wawasaidie kuzifuta tuhuma hizo” amesema Bi. Mokiwa.