Na Lilian Lundo – MAELEZO
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ametaja mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa mpango wa bajeti kwa mwaka 2022/2023 wa wizara yake kuwa ni pamoja na ujenzi wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP), MW 2,115 ambao umefikia asilimia 86.89 ikilinganishwa na asilimia 60.22 za mwezi Aprili, 2022.
Mhe. Makamba ametaja mafanikio hayo, leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
“Mafanikio mbalimbali yamepatikana katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2022/23, ni pamoja na uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umeongezeka kwa asilimia 10.5 na kufikia MW 1,872.05 ikilinganishwa na MW 1,694.55 zilizokuwepo mwaka 2021/22,” amefafanua Makamba.
Mafanikio mengine ni kukamilika kwa Mradi wa Kinyerezi 1 Extension wa MW 185 ambapo mitambo yote minne imewashwa na inachangia MW 185 katika Gridi ya Taifa, ambapo utekelezaji wa mradi huo mwaka 2021/22 ulikuwa umefikia asilimia 88. Vilevile Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Rusumo – MW 80 umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2023, ambapo mwaka 2021/22 ulikuwa asilimia 91.6.
Ameendelea kusema kuwa, Serikali imetoa shilingi bilioni 16.43 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi 6,500 wanaopisha mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga kupitia Mbeya na Tunduma (TAZA) na Wananchi 4,750 tayari wamelipwa fidia zao. Pia ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 132 kutoka Tabora hadi Katavi umefikia asilimia 26.7 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2024.
“Serikali imebadili madeni ya TPDC ya Dola za Marekani bilioni 1.19 na TANESCO ya shilingi trilioni 2.4 kuwa mitaji ya mashirika hayo ili kuvutia uwekezaji pamoja na kuimarisha utendaji na mapato ya mashirika hayo. Vilevile, kimepatikana kibali cha utafutaji wa awali (reconnaissance permit) wa mafuta na gesi asilia katika Kitalu cha Eyasi Wembere kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),” amesema Makamba.
Aidha ametaja mafanikio mengine kuwa ni kufanyika kwa Mjadala wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia tarehe 1 na 2 Novemba, 2022 ambapo matokeo ya mjadala huo ni pamoja na kuandaliwa kwa Dira na Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia utakaozinduliwa mwezi Julai, 2023, pia, uzalishaji wa gesi asilia umeongezeka na kufikia Futi za Ujazo bilioni 68.02 ikilinganishwa na Futi za Ujazo bilioni 59.96 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/22 sawa na ongezeko la asilimia 13.
“Nchi imeendelea kuwa na uhakika wa usalama wa upatikanaji wa mafuta ambapo katika kipindi chote cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 kumekuwepo na akiba ya mafuta ya kutosha,” amefafanua Makamba.
Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Nishati imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya jumla ya shilingi 3,048,632,519,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake.