Na Neema Mbuja, DODOMA
Mhe. Kassim Majaliwa leo Jumanne Mei 30, 2023 ametembelea maonesho ya nishati yanayoendelea jijini Dodoma na kuwataka wafanyakazi wa TANESCO kuendelea kuchapa kazi licha ya changamoto mbalimbali ili kupata mafanikio ya utendaji wao.
Mhe. Majaliwa ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi na watendaji wa taasisi mbalimbali zilizoko chini ya Wizara ya Nishati mara baada ya kutembelea maonesho ya Nishati yanayoendelea kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma ambapo amesema anaridhishwa na utekelezaji na maendeleo ya miradi ya kimkakati kama bwawa la kufua umeme la mwalimu Nyerere unaotekelezwa na TANESCO ambapo mradi umefikia asilimia 86.89.
“Hatuna mashaka na utendaji wenu wa kazi na utaalamu wenu, endeleeni kuchapa kazi, imarisheni utoaji wa huduma, lugha iwe nzuri kwa wateja tutafika tu” alisema Majaliwa
Akimkaribisha waziri mkuu,Mhe. January Makamba Waziri wa Nishati amesema kwa sasa serikali kupitia wizara ya nishati inatoa kipaumbele kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kushirikiana na ofisi ya makamu wa rais ili kuwahamisha wananchi kutumia nishati mbadala na kuhifadhi mazingira
Katika hatua nyingine amepongeza watendaji wa TANESCO wanaofanya kazi kwenye maeneo mbalimbali na kuwataka kuendelea kuwa watoa huduma wazuri kwa wananchi bila kuchoka.
Baadhi ya wabunge waliotembelea kwenye mabanda ya TANESCO kwenye maonesho yanayoendelea mjini Dodoma ni pamoja na Mhe. Anna Lupembe, Mhe. George simbachawene, Mhe. Prof. Paramagamba kabudi, Mhe. Hussein Bashe,Mhe. Hamis Mwinjuma ambapo kwa nyakati tofauti wamesifu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambapo wamesema pindi utakapokamilika utaleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya umeme nchini.