Tume ya madini nchini imetawaka wadau wa madini mkoani Kigoma kutumia fursa ya ujirani mwema kufanya biashara ya madini na wafanyabiashara wa madini kutoka nchi za Kongo na Burundi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo juu ya masuala mbalimbali ya madini mkoani Kigoma katibu mtendaji wa Tume hiyo Mhandisi YAHYA SAMAMBA amesema tayari serikali imefungua milango na kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kushirikiana kwenye shughuli za madini.
Aidha SAMAMBA amewataka wadau hao kuwa wazalendo katika shughuli zao ikiwemo kuhepuka kutorosha madini .
Kwa upande wao baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi wameiomba serikali kuweka utaratibu mzuri wa kuratibu shughuli zao ili kuwawesha kunufaika zaidi na kazi hiyo.
Mafunzo hayo ya siku mbili yamelenga kuwajengea uwezo wadau wa madini mkoani humo kuzifahamu fursa na sheria zinazosimamia sekta ya madini nchini.