Na John Mapepele
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa Kazi nzuri inayoifanya ya kuhifadhi raslimali kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye huku wakisisitiza ushirikishwaji wa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
Wakichangia hoja zao kwenye semina maalum ya uhifadhi iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii leo Mei 29,2023 wabunge hao wamefafanua kuwa katika kipindi kifupi kumekuwa na maboresho makubwa katika uhifadhi wa raslimali ambapo wameomba juhudi zaidi zifanywe ili sekta hizo ziweze kutoa mchango zaidi katika uchumi wa taifa.
Mhe. Ester Matiko amempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mohamed Mchengerwa kwa kuweza kushughulikia mgogoro wa mipaka baina ya hifadhi ya Serengeti na vijiji vinavyoizunguka Hifadhi hiyo kwenye wilaya ya Tarime ambapo amesema njia aliyoitumia ya ushirikishwaji ndiyo njia pekee inayoleta matokea chanya.
Akichangia katika semina hiyo, Mhe. Charles Mwijage ameiomba Wizara kuzingatia sheria na kuondoa mifugo yote ambayo imevamia maeneo mbalimbali ya hifadhi ambapo Mhe. Mchengerwa ametoa siku kumi na nne kuondoa mifugo yote.
Mbunge wa Manyoni Mashariki, Mhe. Pius Chanya ameishauri Serikali kuweka mikakati kabambe ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho makubwa katika mfumo wa taasisi zinazoshughulikia sekta ya utalii kwa kubadili Bodi ya Utalii kuwa Mamlaka.
Awali akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema migogoro mingi inayojitokeza sasa kwenye maeneo ya hifadhi ni siyo ya maliasili na utalii bali imezalishwa na migongano ya sheria ambapo ammewasihi wabunge kuangalia namna bora ya kutunga sheria zinazokinzana.
Hata hivyo amefafanua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Duniani zenye idadi kubwa ya Bioanuai ya Wanyamapori na Mimea. Asilimia 55 ni maeneo yenye Misitu ya asili na misitu ya kupandwa ya Serikali, Makampuni na watu binafsi. Aidha, Tanzania imetenga asilimia 32.5 ya ardhi yake kwa ajili ya uhifadhi wa rasilimali ya Wanyamapori. Vile vile Tanzania ina maeneo ya malikale 132 na vituo 7 vya makumbusho ya Taifa.
Amesema Sekta hizo zina mchango mkubwa katika pato la Taifa ambapo ameeleza kuwa, Utalii ambao kwa kiasi kikubwa unategemea Wanyamapori unachangia asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni na huzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja takribani milioni 1.6.
Aidha, amesema rasilimali za misitu na nyuki huchangia asilimia 3.3 ya pato la Taifa, asilimia 5.9 ya mapato yatokanayo na biashara ya nje, na ajira takribani milioni 3 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Pamoja na faida hizo, hifadhi za Wanyamapori na Misitu ni muhimu sana kwa mifumo ikolojia ikiwa ni pamoja na uhifadhi wa bioanuai, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hewa safi na kuhifadhi vyanzo vya maji.
Ameongeza kuwa Sekta hizi zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, ujangili, uvunaji haramu wa mazao ya misitu, uchimbaji haramu wa madini, uvamizi wa maeneo ya hifadhi kwa ajili ya shughuli za kulisha mifugo, kilimo na makazi na mioto haramu.
Aidha, wadau wa sekta hizi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na changamoto za kikodi, mabadiliko ya sera za kigeni hususan vikwazo kwenye kuingiza nyara za Tembo na Simba kwenye Mataifa ya Ulaya na Marekani na mabadiliko ya Sheria na Kanuni za fedha.