Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Japhet Justine, akifungua mkutano wa Wataalamu 30 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, unaofanyika jijini Arusha.
Mchumi wa Wizara ya Fedha na Mipango kutoka Tanzania, Bi. Jackline Byelembo, akizungumza jambo, wakati wa mkutano wa wataalamu 30 kutoka Wizara za Fedha na Benki Kuu za nchi za Kusini mwa Afrika unaoangazia mikopo ya ndani, unaofanyika jijini Arusha.
Mjumbe kutoka Zimbabwe, Bw. Tapiwa Furusa, akizungumza jambo, wakati wa mkutano wa wataalamu 30 kutoka Wizara za Fedha na Benki Kuu za nchi za Kusini mwa Afrika unaoangazia mikopo ya ndani, unaofanyika jijini Arusha.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Wizara za Fedha na Benki Kuu za nchi za Kusini mwa Afrika wakiwa katika mkutano unaoangazia mikopo ya ndani, unaofanyika jijini Arusha.
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Japhet Justine akiteta jambo na mjumbe kutoka Sudani Kusini, Bw. Lino Akeshak, baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa wataalamu 30 kutoka Wizara za Fedha na Benki Kuu za nchi za Kusini mwa Afrika unaoangazia mikopo ya ndani, unaofanyika jijini Arusha.
Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Japhet Justine (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka nchi za kusini mwa Afrika, waliohudhuria mkutano unaoangazia mikopo ya ndani, unaofanyika jijini Arusha. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Arusha)
….
Na. Peter Haule, WFM, Arusha.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba, amesema kuwa nchi za Kusini mwa Afrika zinaangalia namna ya kuendeleza soko la ndani la mitaji kwa kutumia Hati fungani ili kuziwezesha kupata mikopo ya ndani wakati ambao mikopo mingi ya kibiashara Duniani imekuwa ikipatikana kwa gharama kubwa.
Hayo yamebainishwa jijini Arusha kwa niaba yake na Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Japhet Justine, wakati wa Mkutano wa Wataalamu wa masuala ya uchumi na fedha wanaosimamia madeni ya nchi zao kutoka nchi 16 za kusini mwa Afrika.
Alisema kuwa nchi za kusini mwa Afrika zinaangalia namna ya kutumia Soko au Hati fungani za ndani ambazo ni za muda mfupi, wa kati na mrefu zinatoa nafuu kubwa kwa nchi za Afrika, kwa kuwa mikopo ya aina hiyo ni nafuu na haihitaji matumizi ya dola wala uwekezaji wa nje na haina shinikizo wakati huu ambao soko la Dunia halifanyi vizuri.
“Duniani mikopo ya kibiashara inapatikana kwa gharama kubwa, hivyo mikopo ya ndani itakuwa sehemu ya hatua muhimu ya kuzisaidia nchi za Afrika kufanikisha ufadhili wa bajeti kwa ajili ya maendeleo yao”, alisema Bw. Justine.
Bw. Justine alieleza kuwa kuliendeleza Soko la ndani la Hati Fungani kunatoa fursa kwa nchi za Afrika kufanya vizuri zaidi, ambapo Tanzania kwa sasa inapata mikopo ya zaidi ya trilioni saba kutoka soko la ndani ambayo husaidia kufanikisha bajeti Kuu ya Serikali.
Aliongeza kuwa zipo nchi ambazo zinafanya vizuri katika bajeti zao kwa kutumia fursa ya soko hilo ikiwemo Namibia ambayo zaidi ya asilimia 80 ya Bajeti yake inatokana na mikopo ya ndani kupitia hati fungani zake.
Alisema Mkutano huo utajadili na kuchambua aina ya hati fungani za ndani zinazotolewa huwa na manufaa katika kukuza uchumi wakati ambao mikopo inapopungua kutoka kwa wakopeshaji wa kimataifa na pia wakati huu ambao Soko la hati fungani la Ulaya limepungua kwa kiasi kikubwa.
Aidha amewataka wajumbe wa Mkutano huo kuhakikisha wanakuwa na majadiliano yenye tija na kubadilishana uzoefu ili kuzisaidia Serikali za nchi zao katika kufikia maendeleo endelevu.
Bw. Justine amezipongeza nchi zote zilizoleta wawakilishi wao na pia amewataka wajumbe wa mkutano kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkutano huo umezishilikisha nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo wenyeji Tanzania, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Malawi, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Sudani Kusini na Ethiopia.