Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya akizungumza na wananchi wa kijiji cha Limamu baada ya kufungua mnada wa kwanza wa zao la ufuta mwaka huu,ambapo kilo moja ya ufuta imeweza kununuliwa kwa shilingi 3701
……
Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa mfumo wa stakabadhi Ghalani nchini Asangye Bangu amesema Taasisi yake imedhamiria kutoa elimu ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa wakulima mkoani Ruvuma ili waweze kuuelewa mfumo huo.
Akizungumza na wakulima wa zao la ufuta katika Kijiji cha Limamu wilayani Namtumbo,Bangu amesisitiza wakulima kutambua kuwa kupeleka mazao kuuzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ni kutafuta bei za kiushindani ili wakulima waweze kupata faida katika mazao yao.
Hata hivyo amesisitiza kuwa wakulima wanatakiwa kutambua kuwa bei ambazo zitapatikana kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani zitategemea na bei zilizopo kwenye soko la dunia katika kipindi husika kwa kuwa wanunuzi pia wananunua mazao kulingana na bei iliyopo kwenye soko.
“Wadau wote wa kilimo tuwashawishi wanunuzi wanunue mazao ya wakulima kwa bei nzuri kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kuachana na mfumo holea kwa kuwa serikali inawaangaikia wananchi kuanzia upatikanaji wa mbolea ya ruzuku na pembejeo za kilimo na kuwatafutia soko la uhakika ili wakulima wapate faida kupitia kilimo’’alisisitiza Bangu.
Wakulima wa zao la ufuta wilayani Namtumbo, wamekubali kuuza zao hilo kwa bei ya Sh.3,701 katika mnada wa kwanza uliofanyika katika kijiji cha Limamu huku wakulima wakiipongeza Serikali kwa kusimamia soko la zao la ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalaniKatika mnada huo jumla ya kampuni 17 yamejitokeza kununua ufuta, ambapo kilo 471,223 zilizokusanywa na Chama cha msingi cha Ushirika (AMCOS) cha Limamu kutoka kwa wakulima ambazo zimeuzwa kupitia mfumo huo.
Wakulima wamesema,mfumo wa stakabadhi ghalani una manufaa makubwa kwao kwa sababu unawasaidia kupata soko la uhakika na bei nzuri tofauti na soko huria ambalo wafanyabiashara wanatumia nafasi hiyo kuwanyonya.
Moses Mapunda amesema,mfumo wa stakabadhi ghalani una faida kubwa kwa mkulima na kama ungeanzishwa muda mrefu wakulima wengi wangeondokana na tatizo la umaskini kwenye familia zao.
Amesema kuwa,mfumo huo ni rafiki kwani tangu ulipoanzishwa umesaidia sana kuhamasisha wakulima wengi kuongeza uzalishaji wa mzao mashambani kwa sababu wana uhakika wa kupata fedha nyingi kupitia shughuli zao za kilimo.
Adam Mapunda, ameiomba serikali kuendelea kuimarisha ununuzi wa mazao kupitia mfumo huo ili kutowapa nafasi wafanyabiashara kununua mazao kwa bei ndogo isiyolingana na gharama halisi ya uzalishaji.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Ngollo Malenya,ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaotaka kununua zao hilo nje ya mfumo wa stakabadhi ghalani. Malenya, ameliagiza jeshi la Polisi wilayani humo kushirikiana na wenyeviti,watendaji wa vijiji na kata kuwakamata na kuwachukulia hatua kali madalali wa ufuta wanaojifanya wafanyabiashara wanaopita vijijini ili kuwarubuni wakulima wauze ufuta kwa bei ndogo.
Amelitaja, lengo la serikali kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani ni kuwasaidia wakulima kuwa na soko la uhakika,kupata bei nzuri na kuiwezesha serikali kuwa na takwimu sahihi za uzalishaji wa mazao.
Mkuu huyo wa wilaya,amewataka wakulima wilayani humo kukataa kuuza mazao kwa bei ndogo na nje ya mfumo huo,badala yake watumie vyama vya msingi vya ushirika(AMCOS)vyenje dhamana ya kukusanya mazao na kuuza kupitia minada mbalimbali katika maeneo yao.
Amewaasa wakulima kubadilika na kutumia fedha wanazopata kubadili maisha yao kwa kujenga nyumba bora na kusomesha watoto wao,badala ya kutumia katika mambo ya anasa ikiwemo unywaji wa pombeAidha amesema,kuanzia msimu mpya wa kilimo 2023/2024 mbolea zitapelekwa kila kijiji ili kurahisisha upatikanaji wake na kuwaondolea usumbufu wakulima wa kufuata mbolea hizo makao makuu ya wilaya.
Awali Afisa shughuli wa Chama kikuu cha Ushirika SONAMCU Zamakanal Komba amesema,mfumo wa uendeshaji wa minada mwaka huu utafanyika vijijini badala ya mjini kama ilivyozoeleka ili kutoa fursa kwa wakulima kutambua na kufahamu namna ya uendeshaji wa minada na bei ya mazao yao.
Amesema,katika msimu wa kilimo 2022/2023 jumla ya minada 12 ya ufuta ilifanyika ambapo wastani wa bei ya juu ilikuwa Sh. 2,900 na bei ya chini ilikuwa ni shilingi 2,800.Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa RuvumaMei 26,2023