***************************************
NA MWAMVUA MWINYI, KIBITI
MKUU wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo amemuelekeza mkurugenzi wa halmashauri ya Kibiti pamoja na mkuu wa wilaya ya hiyo kusimamia ujenzi wa hospital ya kisasa ya wilaya na kuzidisha kasi ya kupeleka vifaa vya ujenzi ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo juni mwaka huu.
Aidha ameitaka idara ya manunuzi kuongeza ushirikiano katika suala hilo pasipo kusiganasigana ilihali kazi hiyo ikamilike kwa muda lengwa.
Akikagua hatua ya ujenzi ulipofikia wa hospital ya wilaya ya Kibiti, kata ya Mtawanya ,Ndikilo aliwapongeza kwa kasi wanayokwenda nayo na kuwaasa kutumia vizuri muda wa mwezi mmoja uliobaki vizuri .
Hata hivyo ,alimuambia mkurugenzi ahakikishe pia transformer linawashwa haraka ambapo litasaidia kurahisisha baadhi ya kazi zinazotegemea umeme na kufanya kazi usiku na mchana.
“Watendaji wafanye kazi na wewe,washirikiane kwenye njia yako,ofisa ununuzi na mganga mkuu wa wilaya muwe kwenye njia moja”
“Kama kuna mtendaji atakukwamisha kupitia njia yako ya kwenda kumaliza ujenzi huu kwa wakati basi mchafulie faili lake ,simple tuu”alisisitiza Ndikilo.
Awali mkurugenzi wa Kibiti ,Alvera Ndabagoye alisema,kati ya halmashauri 67 nchini zilizopokea bilioni 1.5 kila moja,kwa ajili ya ujenzi wa awali wa hospital za wilaya,”:’wao walianza ujenzi mwezi wa tatu na kwasasa ujenzi upo hatua ya linta.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibiti, Gulam kifu ,ana matumaini mwezi mmoja uliobakia watakamilisha ujenzi huo na wamepokea maagizo ya mkuu huyo wa mkoa.