NA JOHN BUKUKU, DODOMA.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imeandaa Mradi wa Maendeleo Yanayoendana na Maboresho ya Usafiri wa Umma (TOD) kwa ajili kuhakikisha mradi wa BRT inakuwa tija kwa Taifa.
Mradi wa TOD umelenga kuboresha maeneo ambayo yapo karibu na miundombinu ya barabara ya mabasi yaendayo haraka kwa kuyapendezesha kwa kujenga nyumba za gorofa pamoja na maeneo ya makubwa ya kufanyia biashara, Makazi na Hoteli.
Akizungumza Mkoani Dodoma hivi karibuni katika semina maalam ya kuwajengea uwezo waandishi habari kuhusu shughuli za taasisi hiyo Meneja wa Mipango na Usafirishaji Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Mohamed Kuganda, amesema kuwa utekelezaji wa mradi TOD utasaidia kuleta abiria katika mabasi yaendayo haraka.
Mhandisi Kuganda amesema kuwa lengo ni kuhakikisha usafiri wa mabasi yaendayo haraka unakuwa endelevu na kuleta faida.
“Mradi wa TOD unawakaribisha wawekezaji ili kuwekeza kwa kujenga maeneo ambayo yapo karibu na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kutokana na mipango maalum ya DART” amesema Mhandisi Kuganda.
Amesema kuwa maeneo ambayo wanatarajia kuanza kujenga ni pamoja na Ubungo, Kariakoo Gerezani, Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na Viwanja wa maonesha ya Biashara Kimataifa Sabasaba.
“Nchi za wenzetu wanaotumia mabasi yaendayo haraka waliaza kutekeleza TOD kabla ya mradi BRT kuanza, sisi tumechelewa lakini tunashukuru baadhi ya maendeleo tayari tumekuta yamejengwa nyumba za gorofa ikiwemo mradi wa Watumishi House pamoja na magomeni kota” amesema Mhandisi Kuganda.
Mhandisi Kuganda amefafanua kuwa utekelezaji wa mradi wa TOD utasaidia kuongeza pato kwa serikali kupitia kodi kwa wafanyabiashara pamoja kuongeza kwa abiria wa Mabasi Yaendayo Haraka.