Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na watumishi kutoka katika idara mbalimbali wakiwa katika kikao cha Baraza kilichofanyika katika Ukumbi wa Jiji la Mwanza.
….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Serikali imeombwa kuweka mifumo rafiki ya upatikanaji wa vyumba vya biashara na vizimba kwenye miradi ya kimkakati ya Soko kuu la Mwanza na Stendi ya nyegezi ili kila mwananchi anayewiwa kufanya biashara apate fursa ya kupata eneo la kufanyia biashara.
Ombi hilo limetolewa leo Jumanne Mei 23, 2024 na Diwani wa Kata ya Igoma Mussa Ngolo, wakati akitoa maoni kwenye kikao Cha baraza la madiwani kilicholenga kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji ngazi ya kamati kipindi cha robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema kigezo cha kwanza kilichopendekezwa na Halmashauri ni lazima mfanya biashara awe na leseni ndipo aweze kufanya biashara katika maeneo hayo kitendo ambacho kitawanyima fursa wananchi wengine ambao wanatamani kuitumia miradi hiyo kwaajili ya kujipatia kipato.
“Miradi hii ya Soko na Stendi itakapoanza kufanya kazi itasaidia kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla hivyo ni vyema Halmashauri ipitie upya taratibu za upatikanaji wa vyumba na vizimba ili wananchi waweze kunufaika na kuifurahia miradi hiyo”, amesema Ngolo
Kwa upande wake Naibu Meya wa Jiji la Mwanza Bhiku Kotecha, amesema miradi ya mbalimbali ya kimkakati iliyopo na inayoendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Mwanza ni kwaajili ya wananchi hivyo taratibu za kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na miradi hiyo zitatekelezwa.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Erick Mvati, amesema ugawaji wa vyumba na vizimba unafanywa kwa mujibu wa sheria na kanuni lakini kutokana na maombi ambayo yametolewa kwenye kikao cha baraza la madiwani watafanya marekebisho katika sheria hizo ili wananchi waweze kujitokeza kufanya biashara katika maeneo hayo.
Amesema mradi wa Soko kuu utakapo kamilika utaweza kuchukua zaidi ya wafanyabiashara 1400 na hadi sasa uko asilimia 87 ya ujenzi huku mradi wa Stendi ya nyegezi unatarajiwa kufunguliwa hivi karibuni.