************************************
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri wa Sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mkutano huo utafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), kuanzia tarehe 21 hadi 25 Oktoba, 2019.
Madhumuni ya mkutano huu ni pamoja na kuangalia mwenendo wa hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi; kubainisha utekelezaji wa mikakati ya hifadhi na usimamizi wa mazingira; kupitia Mkakati wa SADC wa Uchumi wa Bahari (SADC Strategy on Blue Economy); na kutathmini maendeleo katika sekta za misitu, wanyamapori na utalii.
Mkutano wa Mawaziri wa sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii utatanguliwa na mikutano ya wataalam wa sekta ya wanyamapori utakaofanyika tarehe 18 hadi19 Oktoba, 2019. Aidha, Mkutano wa Makatibu Wakuu wa sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii utafanyika tarehe 21 hadi 24 Oktoba, 2019. Mikutano hii miwili itajadili na kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa katika kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 25 Oktoba, 2019 kwa maamuzi na maelekezo.
Mkutano wa Mawaziri unatarajiwa kufunguliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ijumaa Oktoba 25, 2019, ukumbi wa AICC, Arusha. Aidha Mkutano wa Makatibu Wakuu unatarajiwa kufunguliwa na Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Oktoba 21, 2019 katika ukumbi wa AICC, Arusha.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 16 wanachama wa SADC wanaotekeleza Mkakati wa SADC kuhusu Usimamizi wa Sheria na Vita Dhidi ya Ujangili wa Wanyamapori (SADC Law Enforcement and Anti-poaching). Maeneo mengine yanahusu Programu za uhifadhi yaliyovuka mpaka wa nchi moja hadi nyingine kwenye maeneo ya misitu, uvuvi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi; utalii; ukuzaji viumbe maji na Mkakati wa Ubora wa Afya wa wanyama wa majini (SADC Transfontiers Conservation Areas; forestry; fisheries; environment and climate change; tourism; regional Aqua-culture strategy and action plan; and SADC Aquatic Animal Health Strategy) pamoja na Programu ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi (Environment and Climate change Program).
Ili kufanikisha mkutano huu sekta ya habari ni muhimu kuhabarisha umma kuhusu masuala yote muhimu yatakayojadiliwa hususan yanayohusu maendeleo ya Mazingira, Maliasili na Utalii kwa nchi wanachama. Serikali inatoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na Mikoa ya jirani kuchangamkia fursa za kibiashara kutokana na kuwepo kwa wageni hao.
Mkutano wa Mawaziri wa Sekta za Mazingira, Maliasili na Utalii ni muendelezo wa mikutano itakayofanyika nchini katika kipindi cha mwaka mmoja ambacho Tanzania ni Mwenyekiti wa jumuiya hiyo.
Mapema mwezi Agosti mwaka huu, Serikali ya Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Dar es Salaam. Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikabidhiwa na kupokea rasmi jukumu la uenyekiti wa Jumuiya hiyo.
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ni moja kati ya jumuiya za kikanda katika bara la Afrika. Jumuiya hii iliundwa kwa dhumuni la kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uchumi, ulinzi , siasa na usalama. Jumuiya hii inaundwa na nchi wanachama 16 ambazo ni: Angola, Botswana, Comoros, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.