Home Mchanganyiko WAZIRI NDALICHAKO ATOA SIKU 15 KWA MSHAURI ELEKEZI BICO KUFANYA TATHMINI YA...

WAZIRI NDALICHAKO ATOA SIKU 15 KWA MSHAURI ELEKEZI BICO KUFANYA TATHMINI YA GHARAMA ZA UJENZI CHUO CHA UALIMU KABANGA

0

Injinia wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga akimuonesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako namna chuo cha Ualimu Kabanga kitakavyoonekana baada ya ujenzi kukamilika

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu, Kabanga unaojengwa na Wizara kupitia Mradi wa TESP wilayani Kasulu mkoani Kigoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga Kasulu Mkoani Kigoma

Muonekano wa sasa wa hatua ya ujenzi wa baadhi ya majengo katika eneo la mradi wa Chuo cha Ualimu Kabanga wilani Kasulu Mkoani Kigoma

………………..

 

Wakati Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga kilichopo Wilayani Kasulu mkoani Kigoma ukiendelea kwa kusuasua Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku 15 kwa Mshauri Elekezi BICO kupitia upya gharama za ujenzi wa mradi huo ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni kumi ili kujiridhisha kama fedha hiyo inaendana na ukubwa wa mradi.

Prof. Ndalichako ametoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo ambapo pamoja na kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi ametilia shaka gharama ya ujenzi ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni kumi kutumika ndivyo sivyo kutokana na aina ya majengo yanayojengwa katika chuo hicho kuwa ya thamani ndogo.

“Hivi ni vighorofa mtoto na narudia ni vighorofa mtoto huwezi kuniambia kwamba majengo haya ambayo kwanza ni machache, pili siyo ghorofa zile kubwa kama tulizojenga katika miradi mingine tena kwa gharama ndogo ya shilingi bilioni sita zinazidiwa na vighorofa hivi hapa kuna kitu hakipo sawa nataka ndani ya siku kumi na tano gharama za mradi zipitiwe upya kwa kila jengo na nipewe taarifa vinginevyo mratibu wa miradi hii utafute kazi nyingine,” alisema Prof. Ndalichako.

Kuhusu kusuasua kwa Mradi Waziri Ndalichako amemtaka Mkandarasi huyo ambaye ni Kampuni ya SUMA JKT kuongeza kasi ya kufanya kazi akisisitiza ziletwe mashine za kisasa ambazo zitarahisisha kazi pamoja na kuongeza vibarua kwenye eneo la kazi.

“Huwezi kutekeleza mradi wa zaidi ya shilingi bilioni kumi kama nyumba yako unayojenga, yaani una kamashine kamoja tena kakusukuma,vibarua wenyewe inaonekana umewaleta leo baada ya kusikia nakuja kukagua, hii haikubaliki tunataka kazi ifanyike usiku na mchana kwa sababu pesa zipo lazima mradi ukamilike haraka,” alisema Waziri Ndalichako.

Mapema akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Ujenzi SUMA JKT, Luteni Kanali Onesmo Njau amesema mpaka sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia thelathini na kudai kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo usumbufu wa kupata vifaa vya ujenzi kama saruji na mchanga.

“Mheshimiwa Waziri tulikuwa tukitegemea kupata saruji kwa kampuni ya Dangote lakini kwa sasa inabidi tufuate wenyewe Dodoma na hivyo kutumia muda mwingi kusubiri vifaa vifike kwenye eneo la mradi,” alisema Kanali Njau.

Naye mshauri elekezi wa mradi huo kutoka BICO, Fred Munishi amekiri kuwa kazi inasuasua na kusema kuwa tayari ametoa maelekezo kwa Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi taarifa ambayo hata hivyo imeonekana kukinzana na taarifa ya Mkandarasi na hivyo kutakiwa kufanya kazi kwa karibu na Mkandarasi.

“Inaonekana hapa hakuna maelewano mazuri baina ya Mkandarasi na mshauri elekezi, sitaki mivutano kazini kaeni pamoja fanyeni kazi ya serikali na mkiendelea hivi tutawaondoa,” alisema Waziri Ndalichako.

Akiwa katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Waziri Ndalichako pia amekagua miradi mingine minne ya elimu katika shule za sekondari na msingi za Kigodya, Ruhita, Nyantare na Kasyenene na kueleza kuridhishwa na kazi huku akisisitiza kuwa serikali inatoa fedha ili kuona matokeo.

Katika ziara hiyo Waziri Ndalichako aliambatana pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dkt. AveMaria Semakafu pamoja na Mratibu wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo pamoja na ule wa TESP