Wanafunzi pamoja na wananchi mbalimbali walipotembelea banda la Chuo cha Bandari Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza maswala mbalimbali kuhusu chuo hicho.
Mkuu wa chuo cha Bandari Dar es Saalam,Dk Lufunyo Hussein akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho hayo jijini Arusha.
….
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Chuo cha Bandari Dar es Salaam kimejiwekea mkakati wa kujenga chuo kikuu kingine kikubwa kitakachohudumia nchi zote zinazozunguka kusini mwa Afrika ifikapo mwaka 2024.
Aidha mikakati mingine ni kuhakikisha wanaendelea kuandaa wataalamu katika sekta ya mafuta na gesi kwani chuo hicho ni chuo cha kimkakati kinachotoa mafunzo mbalimbali ikiwemo kozi za usalama katika sehemu za kusimamia maswala ya gesi pamoja na wataalamu wanaoendesha dhana nzito.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkuu wa chuo cha Bandari Dar es Salaam , Dk Lufunyo Hussein wakati wa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya mafunzo ya ufundi stadi yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Dt Lufunyo amesema kuwa ,wamekuwa wakitoa kozi za muda mfupi na muda mrefu katika kuwaandaa wataalamu katika maswala ya mafuta na gesi ambao wamebobea katika kufanya shughuli hizo kwa ufanisi na umakini mkubwa .
Amebainisha kuwa, chuo hicho ni chuo pekee ambacho kimejengea uwezo Bandari ya Zanzibar na kimekuwa kinafanya nao kazi kwa karibu sana katika maswala mbalimbali.
“Chuo hiki kimejiwekea mikakati ya kuingia mashirikiano na Taasisi za mafunzo katika Bandari zilizopo nchi za nje lengo kubwa likiwa ni kubadilishana uzoefu.”amesema .
Aidha ameongeza kuwa,tayari wataalamu kutoka Antwerp -Ubelgiji walishakuja kwetu kwa ajili ya kuhamisha ujuzi wao na maarifa mbalimbali na namna wanavyofanya kazi zao.
Akizungumzia kuhusiana na uwiano wa wanafunzi wa kike katika chuo hicho amesema idadi ya wanaume ni kubwa kuliko wanawake ambapo wasichana ni asilimia 40 huku wavulana wakiwa ni asilimia 60 kutokana na dhana ya hapo awali kulionekana ubebaji wa mizigo ulikuwa ukitumia nguvu,wakati sasa hivi wanatumia teknolojia maalumu.
Aidha amesema kwa sasa wanawakaribisha wanafunzi wa kike katika kuendesha zana nzito pamoja na kazi zingine za bandari kutokana na sasa shughuli nyingi hufanywa kwa kutumia mitambo.
Aidha ametoa wito kwa vijana kuitumia mitandao vizuri kwa kujifunza maswala mbalimbali ya teknolojia badala ya kuitumia kwa maswala ya tofauti ambayo mwisho wa siku inawaharibia malengo yao.