Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza wakifanya upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu ya moyo wa mtoto wakati wa kambi maalum ya siku tano ya upasuaji wa moyo iliyomalizika leo katika Taasisi hiyo.
Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya siku tano ya upasuaji wa moyo iliyofanyika JKCI.
……
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam.
Watoto 427 wenye matatizo ya matundu kwenye moyo, matatizo ya mishipa ya damu na Valve za moyo wamefanyiwa uchunguzi na upasuaji katika kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto iliyomalizika leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo ya siku tano ya upasuaji wa moyo kwa watoto ilianza tarehe 12/05/2023.
Dkt. Angela alisema kambi ya upasuaji wa moyo ilifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo ya watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka mradi wa Little Heart wa Shirika la Muntada Aid lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza.
Alisema wataalam hao kutoka Shirika la Muntada Aid walikuja nchini na vifaa vyao vilivyotumika katika upasuaji huo wa watoto vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500.
“Watoto 427 wamefanyiwa uchunguzi wa moyo ambapo kati yao watoto 41 wamefanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo ambao unafanyika kwa kutumia mtambo wa Cathlab na watoto 18 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua”.
“Watoto waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri kuna ambao wamesharuhusiwa kurudi nyumbani na wengine wametoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kwenda wodini kuendelea na matibabu ya dawa na mazoezi”, alisema Dkt.Angela.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delila Kimambo aliwashukuru wataalam wa JKCI na wenzao wa Shirika la Muntada Aid kupitia mradi wa Little Heart ambao wamefanikisha upasuaji wa watoto waliokuwa wanasumbuliwa na magonjwa ya moyo.
“Ninalishukuru Shirika la Muntada Aid kupitia mradi wao wa Little Heart ambao wamefanikisha kambi hii ya uchunguzi na upasuaji wa moyo kwa watoto 427, JKCI imejifunza vitu vingi kutoka kwenu na ninaamini mtarudi tena mwezi wa kumi na moja mwaka huu kwaajili ya kuwahudumia watoto wa kitanzania wenye matatizo ya moyo”, alisema Dkt. Delila.
Meneja mradi wa Shirika la Muntada Aid Kabir Miah alisema shirika hilo limekuwa likitoa huduma mbalimbali zikiwemo za afya, elimu na misaada ya kibinadamu katika nchi 22 na hadi sasa zaidi ya watu 262,000 wamenufaika na huduma hizo.
“Shirika la Muntada Aid kupitia mradi wa Little Heart limekuwa likifanya kambi maalum za matibabu ya kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambapo kwa wakati mmoja tunatoa huduma hii kwa watoto 50 hadi 60 lakini katika maeneo mengine idadi inaweza kuongezeka”.
“Tunawataalam wa afya katika nchi mbalimbali ambao wanashirikiana na wataalam wa Hospitali tunayokwenda kutoa huduma ya upasuaji. Licha ya kufanya upasuaji wataalam wetu pia wanatoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wenzao wanaofanya nao kazi ili nao waweze kutoa huduma kama zao”, alisema Kabir.
Nao wazazi ambao watoto wao walitibiwa katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa kujenga Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kusomesha wataalam na kununua vifaa tiba vya kisasa ambavyo vimewasaidia watoto wao kupata huduma ya upasuaji hapa nchini.
Diana Kulwa kutoka mkoa wa Mwanza alisema mtoto wake alikuwa na tatizo la tundu kwenye moyo na aligundua kuwa na tatizo hilo akiwa na umri wa miaka mitatu na baadaye alipata rufaa kutoka hospitali ya Bugando na kupelekwa JKCI kwaajili ya kupata matibabu ya kibingwa.
“Ninashukuru sana kwa huduma niliyoipata kwani sikuwa na fedha za kulipia matibabu ya mwanangu lakini nimepata msamaha wa matibabu na mwanangu kafanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri”.
“Niliambiwa gharama za matibabu ni milioni nane na laki tano kwa kuwa sina uwezo nimechangia shilingi laki tano na mwanangu kafanyiwa upasuaji. Ninaishukuru sana Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kunihurumia na kumtibu mwanangu”, alishukuru Diana.
Shija Matunda aliwaomba kinamama wenye watoto walio na matatizo ya moyo wasiogope na kukata tamaa kwani huduma za upasuaji zinapatikana hapa nchini hata kama mtu hana uwezo wa kulipia anapata huduma kwani ukifika hospitali utaelekezwa utaratibu wa kufuata.
“Ninawaomba kina mama wenzangu kuwaleta watoto wao katika matibabu mwanangu alikuwa anapumua haraka haraka baada ya kufanyiwa uchunguzi alikutwa na tundu kwenye moyo, amefanyiwa upasuaji anaendelea vizuri”, alisema Shija.