Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka mamlaka zilizozifungia baadhi ya hoteli za kitalii katika jiji la Arusha kuangalia namna ya kuzifungulia ili zisaidie kupokea wimbi kubwa la watalii wanafurika katika msimu huu huku akitoa maelekezo mahususi kwa Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kuweka taa za barabarani, kujenga Arena na jengo la vivutio mbalimbali vya utalii kwa haraka ili kuboresha utalii.
Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo wakati akikabidhi pikipiki 15 kwenye Kituo cha Polisi cha Diplomasia ya Utalii jijini Arusha zilizotolewa na Benki ya CRDB zitakazosaidia askari kufanya doria ili kuwasaidia kuimarisha usalama wa watalii huku akielekeza mifumo ya usalama ya utalii iliyofungwa kwenye taasisi mbalimbali za Wizara ya Maliasili na Utalii, ziunganishwe na kituo hicho ambapo pia ameahidi Serikali itatoa Gari aina ya Toyota LandCruiser kwa lengo hilo hilo.
“Kwa hiyo niwaombe Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya zile hoteli ambazo zimefungwa hapa Arusha, sasa ni wakati Serikali tuchukue hatua, hoteli hizo zifunguliwe ili wageni wanaokuja waweze kupata sehemu za kukaa wakifika hapa nchini.” Amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Aidha, ameziomba Benki kufikiria kuwakopesha wawekezaji ambao wanataka kuwekeza katika kujenga hoteli huku akifafanua kuwa wakitoa mikopo katika eneo hilo hawawezi kupata hasara kwa kuwa kwa sasa kumekuwa na hitaji kubwa la hoteli za kupumzikia watalii kutokana na uwingi wa wageni wanaokuja kutembelea Tanzania baada ya juhudi alizofanya Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya Royal tour.
“Lakini niziombe benki, mkitoa fedha kwenye uwekezaji wa hoteli hamjapoteza hata kidogo maana kule Karatu zimejengwa hoteli za nyota tano nje ya Hifadhi lakini hakuna nafasi hadi mwezi wa kumi na gharama za kulala siyo ndogo nyingine zina kwenda hadi dola 12000 kwa siku lakini zimejaa.” Amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Ameongeza kuwa katika kipindi hiki Serikali inakwenda kufanya maamuzi ya haraka na yakizalendo katika misingi ya sheria na kanuni katika uwekezaji na kwamba atakaye chelewesha au kwamisha kufanya maamuzi ataondolewa mara moja.
Aidha, amesema anatambua hapo awali maeneo ya Serikali ya uwekezaji yalikuwa yakiongozwa kwa rushwa ambapo kwa sasa amesisitiza kuwa maafisa hao wataondolewa ili kuwaweka watu waadilifu.
Mhe. Waziri pia ameelekeza TANAPA kuboresha kituo hicho kwa kujengea vitofali vya katika uwanja wa kituo na Hifadhi ya Ngorongoro kupiga rangi ukuta wote wa kituo huku TFS wakielekezwa kuja na aina nzuri za miti ambazo zitapandwa na kuleta mandhari nzuri.