Tanzania imeungana na nchi nyingine Duniani katika kuadhimisha siku ya Makumbusho Duniani inayoadhimishwa Kila Tarehe 18 Mei, kwa kushirikiana na Ubalozi wa India hapa nchini.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika Kijiji cha Makumbusho, Dar es Salaam, Naibu Balozi wa India Mhe. Mojar Varma amepongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT) kwa kazi nzuri ya uhifadhi wa urithi wa asili na Utamaduni jambo linalotoa nafasi kwa vizazi vya sasa na vijavyo kunufaika na Urithi huo kwa ustawi na maendeleo endelevu.
Mhe Varma ameongeza kuwa Tanzania na India zimekuwa na mahusiano mazuri pia zimekuwa zikishirikiana vyema katika nyanja mbalimbali hususan utamaduni, hivyo ushiriki wa Ubalozi huo kwenye maadhimisho hayo makubwa Duniani ni alama ya kuendendeleza udugu huko.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Lwoga amealeza kuwa kwa Mwaka 2023 Taasisi imeadhimisha siku hiyo kwa zoezi la upandaji miti, program za kielimu, maonesho ya wajasiriamali, burudani ya ngoma za asili nchini na muziki wa asili ya nchini India huku vituo vingine vya Makumbusho nchini vikiendesha program mbalimbali za kielimu pamoja na kukutana na wadau wa utalii.
Dkt. Lwoga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuzitembelea Makumbusho za Taifa ili kunufaika na elimu, burudani kupitia maonesho na mikusanyo iliyohifadhiwa na kuoneshwa kwenye matawi yote ya Makumbusho nchini.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuti ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour na Wizara chini ya Mhe. Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbas kwa kuweka mikakati ya kuendeleza juhudi za kutangaza Utalii wa makumbusho na Malikale.
“Kupitia juhudi hizo Makumbusho imeweza kupokea wageni zaidi ya milioni moja waka 2022”. amesema Dkt. Lwoga.