NAIBU katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde akimkabidhi cheti Mtendaji Mkuu wa mtandao wa Fullshangweblog Bw. John Bukuku mara baada ya kupokea Mafunzo ya siku Tano kuhusu majukumu ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART yaliyofanyika kwenye hoteli ya Dodoma City jijini Dosoma katikati ni Mtendaji Mkuu wa DART Dkt Edwin Mhede.NAIBU katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde akifunga Mafunzo hayo Kwa waandishi wa habari yaliyofanyika Kwa siku Tano kwenye hoteli ya Dodoma City jijini Dosoma.
Mtendaji Mkuu wa DART Dkt Edwin Mhede akizungumza wakati wa kufunga Mafunzo hayo yaliyofanyika Kwa siku Tano Katika hoteli ya Dodoma City jijini Dodoma.
Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI
NAIBU katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde amewataka waandishi wa habari nchini kuendelea kuuhabarisha umma juu ya miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha na kurahisisha maisha ya watanzania kama ilivyo kwa mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka(DART).
Dkt.Msonde ameyasema hayo Mei 18, 2023 jijini Dodoma alipokuwa akifunga mafunzo elekezi kwa waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa mradi wa DART kwa niaba Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejembi.
Naibu Katibu huyo amesema Wakala huo ni muhimu kwa usafiri wa Jiji la Dar-es-salaam hivyo ni jukumu la waandishi wa habari kuhakikisha mpango mkakati wa DART unaeleweka kwa wadau ili kupunguza changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika uendeshaji wa Wakala huo.
Amewataka waandishi hao kuhakikisha wanaeleza mafanikio yaliyofikiwa na wakala huo kwa wadau ili kuleta mafanikio makubwa katika nchi ya Tanzania na hasa wananchi wanapokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu miradi mbalimbali ya serikali.
“Lengo kuu la mafunzo ni kuwajengea uelewa wa pamoja kuhusu namna mradi wa unavyofanya kazi, miundombinu yake ,changamoto zilizopo na namna bora ya utatuzi wa changamoto hizo hivyo ni wajibu wenu kuuhabarisha umma kuhusu utekelezaji wa kazi za wakala huu,”amesema.
Amewaasa kuwa mabalozi wazuri wa mradi na pale inapotokea mtu anatoa taarifa zisizo sahihi za mradi kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kusaidia kutoa ufafanuzi,
“Niwaombe mkawe mabalozi wazuri wa miradi mingine inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi mahiri wa Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”amesisitiza Dkt. Msonde.
Aidha, ametoa rai kwa Taasisi nyingine hasa zile ambazo ziko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuona umuhimu wa kuwashirikisha waandishi wa habari katika shughuli zao ili kufikisha taarifa kwa wananchi.