……………………………………………
Na Dotto Mwaibale, Sinida
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Isdor Mpango anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya siku ya nyuki duniani kwa mwaka 2023
ambayo yatafanyika May 21, 2023 mkoani Singida katika viwanja vya Bombadia.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter
Serukamba wakati akitoa taarifa ya maadhimisho hayo kwa waandishi wa habari ambapo
alisema yatakuwa kwa muda wa siku nne kuanzia kesho May 18, 2023 hadisiku ya
kilele chakeMay 21, 2023 chini ya Kauli mbiu isemayo “Tuwalinde Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Usalama wa Chakula“
“Leo
nimewaalika hapa kwa lengo moja kuu nalo ni kuzungumzia maadhimisho ya siku ya
nyuki duniani kitaifa kwa mwaka huu wa 2023. Maadhimisho haya ni utekelezaji wa
azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la Disemba 20, 2017 ambalo lililenga kutambua mchango wa mdudu nyuki katika
usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira,” alisema Serukamba.
Serukamba alisema maadhimisho hayo yatajumuisha matukio
mbalimbali kama, maonesho ya bidhaa na
huduma za ufugaji nyuki ambapo wadau wataweza kufahamu faida za mazao
zaidi ya sita yanayopatikana kutoka kwa mdudu nyuki na kampeni ya utundikaji mizinga
itakayofanyika Wilaya ya Itigi katika Kijiji cha Kitaraka kwa lengo la
kuwajengea wananchi uelewa kuhusu mbinu bora za ufugaji nyuki.
Alitaja mambo mengine yatakayofanyika ni safari maalumu
zilizo andaliwa kwa lengo la kuweza kutembelea vivutio vilivyopo katika mkoa
wetu wa Singida safari zilizopewa jina la ’Nyuki Safari’ na semina zitakazo husisha elimu ya mambo
muhimu katika ufugaji nyuki mfano namna ya kuongeza ubora wa mazao ya nyuki na
mwisho ni tukio la sherehe za kilele zitakazofanyika May 21, 2023.
Serukamba alisema maadhimsho ya siku ya nyuki duniani
kufanyika mkoani Singida ni fursa kwa wadau kuweza kujifunza pamoja na mambo mengine
mbinu za kuweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki pia, kuweza kupata masoko
ya mazao ya nyuki. kama inavyofahamika kuwa Mkoa wa Singida umekuwa ukifanya
shughuli za ufugaji nyuki kwa kipindi kirefu na kuweza kuchangia kipato cha
wananchi wa mkoa huo na kuwa wakulima wakubwa wa zao la alizeti nchini wakiwepo
na wa Mkoa wa Singida wameendelea kunufaika na huduma ya uchavushaji kutoka kwa
mdudu nyuki.
Serukamba alitumia nafasihiyo kutoa rai na kuwakalibisha
wananchi wote wa Mkoa wa Singida na mikoa jirani kuweza kushiriki katika
maadhimisho hayo ambayo ni muhimu.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Ufugaji Nyuki,
Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras, akizungumzia umuhimu wa
maadhimisho hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbas alisema
yamelenga kutambua umuhimu wa mdudu nyuki katika uhifadhi wa mazingira na
usalama wa chakula.
Alisema mdudu nyuki ni muhimu sana kwani ni miongoni mwa
wadudu wachavushaji waliopo duniani na uchavusha takribani asilimia 80 ya mazao
yote ya chakula hivyo basi umuhimu wake si katika kuzalisha asali tu bali na
katika utunzaji wa mazingira.
”Mazingira mazuri tunayoyaona,ikiwemo miti, mimea
mbalimbali tunayoiona ikiwa imestawi vizuri na kustawi kwake kuna changiwa kwa
kiwango kikubwa na uwepo wa mdudu nyuki,”
alisema Pancras.
Pancras alisema tukiwa kama sehemu ya watu duniani kila
mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anatunza mazingira ya mdudu nyuki na mazalia
yake na kufurahia uwepo wake kutokana na faida tunazozipata ikiwemo usalama wa
chakula.
Alisema katika maonesho hayo kutakuwa na bidhaa za aina
tofauti tofauti kutoka kwa wadau
mbalimbali ambao watazionesha pamoja na teknolojia
za ufugaji wa nyuki na utunzaji wa mazingira na pia kutakuwa na semina ambazo zimejikita
kuangalia mchango wa mdudu nyuki katika uchavushaji na madhara yanayo tokea
dhidi ya mdudu huyo baada ya kutumia viuatilifu kwa njia ambayo sio sahihi na
kuweza kuwaaathiri wadudu wachavushaji wakiwemo nyuki.
Aidha, Pancras alisema kutakuwa na uangaliaji wa ubora wa
mazao ya nyuki na miongozo mbalimbali inayosimamia sekta ya nyuki na kuwa jambo
kubwa ni ile Siku ya Safari za Nyuki ambayo itatumika kutangaza na kuhamasisha
utalii wa Mkoa Singida.
Alisema Nyuki Safari ni zao jipya ambao ni utalii wa
nyuki ambapo wananchi wote na wadau watakao kuwepo kwenye maadhimisho hayo
wataweza kwenda kutembelea maeneo zinapofanyika shughuli za nyuki na kutembelea
vivutio vya utalii vilivyopo Mkoa wa Singida na kuwa jambo hilo linakwenda
kufungua hamasa ya watu kwenda kuwekeza
katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii na kuwa lengo la wizara hiyo
kushirikiana na mkoa katika maadhimisho hayo lilikuwa ni kuufanya mkoa huo ukue
kiuchumi wakizingatia kuwa upo jirani na makao makuu ya nchi Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras, akizungumzia umuhimu wa maadhimisho hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbas.
Ufugaji bora wa nyuki unavyofanyika.
Muuonekano wa mdudu nyuki.
Bidhaa za nyuki zikiwa sokoni.
Muonekano wa mzinga wa nyuki wa kisasa.
Muonekano wa mabanda ya maonesho ya maadhimisho hayo IDA katika viwanja vya Bombadia vilivyopo Manispaa ya Singida wakati wa maandalizi yake.