Na WAF, Dodoma.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu mapema leo amekutana na Makamu Mkurugenzi wa Misheni ya USAID nchini Tanzania Bw. Alexander Klaits pamoja na ujumbe wake wote kuhusu Mpango wa uratibu na uimarishaji wa huduza zitolewazo na watoa huduma wa afya ngazi ya jamii.
Katika kikao hicho kilichofanyika Ofisi za Wizra Jijini Dodoma, Waziri Ummy amesema watoa huduma za afya ngazi ya jamii wamekuwa kiungo muhimu katika uboreshaji wa huduma za afya nchini kwa mchango wao wanaotoa kuanzia kwenye utoaji wa elimu ya afya pamoja na kushiriki kikamilifu kwenye mapambano ya magonjwa mbalimbali yakiwemo yale ya mlipuko.
“Wizara imeweza kuandaa miongozo ya uendeshaji wa shughuli za watoa huduma za afya ngazi ya jamii kwa kuanzia kada ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii ambayo wataalam hupata mafunzo ya mwaka mmoja chini ya NACTVET na hadi sasa jumla ya watoa huduma 13,400 wamepata mafunzo” amesema Waziri Ummy
Pia, Waziri Ummy amesema kupitia mpango huo, vipaumbele sita vya huduma za afya vitazingatiwa na kutolewa kwa ubora zaidi huku akivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni, kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, lishe, afya na usafi wa mazingira, magonjwa ya kuambukiza (Mlaria, Kifua Kikuu na UKIMWI), Magonjwa yasiyoambukiza pamoja na utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Waziri Ummy amesema ili kuweza kutekeleza kikamilifu vipaumbele hivyo, mchango wa Wadau wa Sekta ya Afya ni muhimu zaidi ili kuboresha ubora wa huduma zitolewazo na watoa huduma za afya ngazi ya jamii.
“Tunahitaji kuunganisha nguvu za pamoja ili kuzalisha watoa huduma za afya walio bora hivyo ni muhimu watumishi hawa wakapata mafunzo ya miezi 6 chini ya vyuo vya mafunzo ya afya kwa kuzingatia mitaala ya Serikali, Wadau kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuajiri na kulipa posho za watoa huduma za afya ngazi ya jamii, kuwawezesha watoa huduma na vitendea kazi ili kuwa na ufanisi wa kazi pamoja na kuimarisha uratibu wa shughulii zao” amesisitiza Waziri Ummy
Kwa upande wake Makamu Mkurugenzi wa Misheni USAID Bw. Alexander Klauts ameipongeza Wizara kwa kuona kipaumbele cha kuboresha utoaji wa huduma za watoa huduma za afya ngazi ya jamii.
Tumekuwa tukishirikiana na mataifa zaidi ya 15 katika eneo hili la uimarishaji wa huduma hizi na sisi tupo tayari kutoa msaada wa kitaalam na rasilimali fedha ili kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya kupitia watoa huduma za afya ngazi ya jamii” amesema Bw. Klauts.