Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewakumbusha wadau mbalimbali wanaojishughulisha na uwekaji na uidhinishaji wa mifumo ya gesi asilia katika magari, kuwasilisha taarifa za shughuli zao katika mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Petroli na Gesi (NPGIS), ili kuiwezesha EWURA na Wizara ya Nishati kuwa na taarifa sahihi zitazowezesha utekelezaji wa jukumu lake la kisheria la kuisimamia sekta ya nishati nchini.
Hayo yamesemwa na Meneja wa EWURA anaye shughulikia Usambazaji Gesi Asilia, Mha. Nkilila Lucas, wakati wa warsha kwa wadau wa gesi asilia iliyokandamizwa inayofanyika katika Ofisi za EWURA Kanda ya Mashariki, jijini Dar es Salaam.
“Mfumo wa Taifa wa Taarifa za Petroli na Gesi (NPGIS) unasimamiwa na EWURA na ulianzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 124 cha Sheria ya Petroli kwa dhumuni la kuratibu taarifa na takwimu zinazohusiana na shughuli za mkondo wa kati na wa chini wa Sekta ya gesi asilia nchini”
“Hivyo basi wadau wenye karakana za kuhuisha mifumo ya magari kutumia gesi asilia iliyokandamizwa, waidhinishaji na wakaguzi wa mifumo hiyo, mliopo hapa leo, mnapaswa kuwasilisha taarifa za kazi zenu katika mfumo.”alisema.
Mha. Nkilila aliongeza kuwa baada ya gari kuwekewa mfumo wa gesi asilia iliyokandamizwa, linapaswa kukaguliwa ili kujiridhisha endapo mfumo huo unakidhi viwango, kisha kuidhinishwa kwaajili ya matumizi, na taarifa za ukaguzi huo ni lazima ziwekwe katika mfumo wa NPGIS.
Nkilila pia, amewataka wadau hao kutoa maoni na kujitahiri kuuelewa vizuri mfumo, sanjari na kutosita kuwasiliana na EWURA kwa changamoto yoyote watakayokuna nayo wakati wa uwasilishaji wa taarifa kwenye NPGIS.
Mfumo wa NPGIS unpatikana katika tovuti ya EWURA www.ewura.go.tz na taarifa zote zinapokelewa kwa njia ya mtandao.