Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernad Membe umesafirishwa leo tarehe 15/5/2023 kwa Helicopter ya Kijeshi kwenda Mkoani Lindi, Rondo Chiponda kwa ajili ya mazishi.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Amri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suruhu Hassani ametoa helicopter mbili kwa ajili ya kusafisha mwili pamoja na waombolezaji kwenda Rondo Chiponda kwa ajili ya mazishi.
Mhe. Membe amesindikizwa kwa heshima kwani ni miongoni mwa wanajeshi walioshiriki vita vya Kagera.
Mhe. Membe amefariki Mei 12, 2023 katika Hospital ya Kairuki (HK) iliyoko Mikocheni, jijini Dar es Salaam, akiwa anapatiwa matibabu, baada ya kupelekwa kutokana na changamoto ya homa na kifua.
Taifa limempoteza mmoja wa Wanadiplomasia, Jasusi na Mwanasiasa mahiri Bernard Membe aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimaitaifa, katika serikali ya awamu ya nne iliyokuwa chini ya Rais Dkt. Jakaya Kikwete.
Membe ambaye anatajwa kama Kachero mbobevu, Mwanadiplomasia nguli na Mwanansiasa makini, aliwahi kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2020, akipeperusha bendera ya ACT Wazalendo.
Historia ya Mwanadiplomasia huyo imeanzia katika Kijiji cha, Rondo, Chiponda, Wilaya ya Lindi Vijijini, ambapo Novemba 9, 1953; katika familia ya mwindaji Kamillius Anton Ntanchile na mkewe Cecilia John Membe, walibahatika kupata mtoto wao wa pili, japo baadaye walizaliwa wengine watano na kuifanya familia kuwa na jumla ya watoto saba.
Waziri huyo wa zamani ni Mmwera, na kama ilivyo desturi ya watu wa kabila hilo, watoto hutumia jina la ukoo wa Mama, na hii ndiyo sababu Bernard na ndugu zake, wamekuwa wanatumia jina la ubini la upande wa mama yao Cecilia, yaani Membe.
Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, baba yake Membe alitamani kazi ya uwindandaji toka akiwa na miaka mitano, na hii ilitokana na ukweli kuwa, alimshuhudia Simba akimkamata na kumrarua mama yake, na hivyo kujiapiza kuwa, akiwa mkubwa atamiliki bunduki na kuwa mwindaji, jambo ambalo alifafanikisha.
Mzee huyu (Baba yake Membe) alifariki dunia mwaka 1987 kwa kuvuja damu nyingi kutokana na kuchelewa kupata msaada wa kitabibu kwa zaidi ya saa 10, baada ya kulipuliwa na bunduki akiwa katika harakati zake za uwindaji.