Watendaji wa Wizara ya Afya Kitengo cha maradhi yasioambukiza wakitoa huduma za awali kwa wananchi waliojitokeza katika zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi lililoratibiwa na Wizara wa Afya Zanzibar wakishirikiana na Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China huko Hospital ya Rufaa Mnazimmoja Mjini Unguja.
Watendaji wa Wizara ya Afya Kitengo cha maradhi yasioambukiza na watendaji wa Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China wakipitia taarifa za awali za wananchi waliojitokeza katika zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi lililoratibiwa na Wizara wa Afya Zanzibar wakishirikiana na Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China huko Hospital ya Rufaa Mnazimmoja Mjini Unguja.
Meneja wa kitengo cha Maradhi yasioambukiza Zanzibar (NCD) Dkt. Omar Muhammed Sleiman akielezea kuhusiana na zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi alipokua akifanya mahojiano na Waandishi wa habari wakati zoezi hilo likiendelea huko Hospital ya Rufaa Mnazimmoja Mjini Unguja .Mei 15,2023.
Mwananchi aliejiotokeza katika zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi Khadija Khamis akifanya mahojiano na Waandishi wa Habari kuhusiana na zoezi hilo lililoratibiwa na Wizara wa Afya Zanzibar wakishirikiana na Hospital ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China huko Hospital ya Rufaa Mnazimmoja Mjini Unguja.
….
Na Rahma Khamis – Maelezo
Jamii nchini imeshauriwa kujitokeza kupima afya zao ili kufahamu kama kuna viashiria vya ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ili kupatiwa tiba mapema.
Ushauri huo umetolewa na Meneja wa Kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (NCD) Dkt Omar Muhamed Suleiman wakati walipokuwa wakiendesha zoezi la uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi katika Kitengo cha maradhi hayo Hospitali ya Mnazimmoja.
Amesema kuwa ugonjwa huo ni tishio kubwa duniani kote kutokana ripoti yaShirika la Afya Ulimwenguni (WHO) inakadiria kuwa zaidi ya wanawake 275,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo ambapo idadi kubwa ya watu hao ni kutoka nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Aidha amefahamisha kuwa iwapo saratani hiyo itagundulika katika hatua za awali ni rahisi kutibika na kupona kabisa hivyo Wizara imeamua kuanzisha uchunguzi huo hatua kwa hatua ili wananchi kuweza kujigundua nmapema na kupatiwa matibabu.
Amesema kuwa lengo la kufanya uchunguzi kwa akina mama na wanawake hao ni kuangalia usalama wa afya zao hasa saratani ya shingo ya kizazi na kupatiwa matibabu ambapo zoezi hilo litafanyika bila ya malipo.
Dkt Omar amefafanua kuwa wanawake wenye umri kati ya miaka 21hadi 65 ambao wamewahi kushiriki tendo la ndoa wanatakiwa kufanya uchunguzi huo ambapo zoezi hilo ni muendelezo wa awamu ya tatu uliyofanyika miezi iliyopita.
Katika hatua nyengine Dkt Omar amefahamisha kuwa tarehe 20 zoezi hilo litafanyika Tumbatu , 22-23 Hospitali ya Kitogani na 24-25 litafanyika katika Hospitali ya Kivunge ambapo zoezi hilo litaendelea hadi juni mosi katika Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja.
Akitaja baadhi ya vichecheo vinavyochangia tatizo hilo Dkt Omar ameeleza kuwa ni kushiriki tendo la ndoa na wanaume tofauti, kuugua magonjwa ya zinaa mara kwa mara pamoja na kutia vitu visivyostahiki sehemu za siri jambo ambalo linahatarisha afya ya uzazi.
Hata hivyo Dkt Omari amewataka akina mama na wanawake kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ili kutambua tatizo linalowasumbua na kupatiwa tiba.
Nao wananchi waliyofanyiwa uchunguzi huo wameiomba Serikali kuendelea kushirikiana na wafadhili mbalimbali katika sekta ya afya ili kuwapatia tiba kwani kufanya hivyo kunawapunguzia gharama za matibu.
Wamefahamisha kuwa hapo nuyma walikuwa wakipata shida kutokana na matibabu ya ugonjwa huo kuwa hayapatikani Zanzibar lakini kwa sasa wamekua wakipatiwa tiba hizo mara kwa mara jambo ambalo limewaondoshea usumbufu waliokuwa wakiupata hapo kabla.
“Tunashukuru sana kufanyiwa uchunguzi huu zoezi linakwenda vizuri wala hakuna maumivu yoyote zamani tulikua tunapata shida lakini baada ya Serikali kuanzisha kitengo cha Saratani na kuwa inatuletea madaktari kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matibau tumeweza kufarajika sihaba ,tunaomba iendeleee kutufikiria zaidi katika maradhi mengine,”walishauri wananchi.
Aidha wamewashauri akina mama wenzao na wanawake kujitokeza kwa wingi kwenda kuangalia afya zao kwa kufanya uchunguzi wa maradhi mbalimbali kwani uchunguzi na matibabu hayo ni bure.
Uchunguzi wa maradhi hayo umeandaliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya wakishirikiana na Hospitali ya Nanjing ya Jamuhuri ya watu wa China .