Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akikabidhi Kombe kwa washindi wa kwanza wa mbio za magari zilizoandaliwa na Chama Cha Iringa Motor Sports Club kwa udhamini wa Shamba la Miti la Sao Hill Mei 14, 2023, alipofunga mashindano ya mbio hizo wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akipokea Tuzo ya kutambua mchango wa Wizara yake katika kuendeleza michezo ikiwemo mchezo wa mbio za magari kutoka Chama cha Iringa Motor Sports Club, Mei 14, 2023 alipofunga mashindano ya mbio hizo wilayani Mufindi mkoani Iringa.
……………………………….
Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika mchezo wa mbio za magari ili kuendeleza mchezo huo.
Mhe. Chana ametoa wito huo Mei 14, 2023 wilayani Mufindi mkoani Iringa wakati akifunga mashindano ya mbio za magari ambapo amewapongeza Waandaji wa Mashindano hayo yajulikanayo kama Iringa Rally ambayo yamejumuisha Madereva takriban 45 kutoka katika mikoa saba ya Tanzania Bara pamoja na washiriki kutoka nchi ya Uganda, Kenya na Zambia.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dkt. Samia, inaendelea na lengo la kuiwezesha Tanzania kuwa na miundombinu ya michezo bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ikiwemo miundombinu ya michezo wa magari, amesema Mhe. Pindi.
Ametumia nafasi hiyo, kulielekeza Baraza la Michezo la Taifa kukaa na wadau wa Mchezo huo ili kuwapa miongozo na taratibu nzuri za kuratibu mashindano hayo ili kuhakikisha vijana wengi wanashiriki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Iringa Motor Sports Club Bw. Amjad Khan, ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono mashindano hayo ambayo yamekuwa na mwitikio mzuri kwa jamii.