Prof. Dominique Uwizeyimana, Kutoka Chuo Kikuu cha Johanesburg, akiwasilisha mada katika Kongamano Kongamano la Kimataifa kuhusu masuala ya Utawala bora, Uongozi na mabadiliko ya Kiuchumi kwa Jamii
Baadhi ya washiriki wakisiliza kwa makini wasilisho wakati wa Kongamano
…
Kongamano la Kwanza la Kimataifa kuhusu masuala ya Utawala bora, Uongozi na mabadiliko ya Kiuchumi kwa Jamii, limeanza leo jijini Dar es Salaam, likikutanisha zaidi ya wataalamu 80 katika masuala ya Uongozi na Utawala Bora, kutoka nchi tisa za Afrika, Ulaya na Asia.Kongamano hili la siku tatu, linafanyika katika Hoteli ya Seascape, Mbezi Beach; kwa kuandaliwa na Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Skuli ya Utawala na Menejimenti kwa Ushirikiano na Chuo Kikuu Cha Kabale nchini Uganda.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kongamano hilo, Mwenyekiti wa Kongamano hilo Dkt. Idda Lyatonga, kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, amesema zaidi ya tafiti 18 katika maeneo mbalimbali ya Utawala, menejimenti na Uongozi, zitajadiliwa na washiriki wa kongamano hilo, na kuyataja baadhi ya maeneo ya utafiti kuwa ni Utawala na Menejimenti katika Vyuo Vikuu, Utawala katika maendeleo ya Jamii kiuchumi, rushwa, Utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ushiriki wa wananchi katika maendeleo, Teknolojia n.k
“Tunategemea kupitia kongamano hili tafiti zaidi zitafanyika, pamoja na kuboresha mawasilisho yatakayofanyika kwa ajili ya kuchapishwa kwenye majarida mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa, kwa lengo la kuongeza uelewa mpana wa masuala ya kiutawala kwa jamii.”
AmesemaAidha kupitia Kongamano hili Dkt. Lyatonga amesema wanategemea kuwa maazimio ambayo yatatokana na mijadala na mawasilisho yatakayofanyika ili kuwasilishwa kwenye ngazi mbalimbali za maamuzi na mamlaka za kiutawala ili kuchagiza mijadala ya kuboresha mifumo ya utendaji, utawala na utoaji haki, pamoja na kuundwa sera zitakazosaidia nchi zetu kuondokana na changamoto mbalimbali za kitawala na maamuzi.
Amesema, kongamano hilo limelenga kuchochea wanataaluma kuongeza bidii katika kufanya tafiti zitakazochochea mabadiliko katika jamii, kuanzisha ushirikiano katika kufanya tafiti pamoja na kuweka mikakati ya pamoja na namna vyuo vikuu vinavyoweka kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu jamii kwa kuhusisha jamii yenyewe.
Zaidi ya Washiriki 75 wanashiriki kongamano hilo kutoka nchi za Rwanda, Tanzania, Kenya, Uganda, Nigeria, Ghana, Afrika Kusini, Zimbabwe, Lesotho, Brazil huku washirika zaidi ya 15 kutoka nchi za USA, Korea Kusini, Canada na UK wakishiriki kwa njia ya mtandao.