Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali inatarajia kubadilisha jina la Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili MIREMBE na kuitwa National Instititue for Mental Health.
Waziri Ummy amesema hayo leo kwenye semina maalum iliyoandaliwa kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata elimu ya masuala ya afya ya akili, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) pamoja na Bohari ya Dawa (MSD)
“Tunakwenda kubadili jina la Hospitali ya Mirembe ili kujenga taswira mpya ndani ya jamii kwenye huduma zinaotolewa pale, mtu anaweza kwenda pale kutibiwa hata Malaria, lakini jamii inamuita ‘chizi’. Tunataka Mirembe iitwe National Instititue for Mental Health” amesema Waziri Ummy Mwalimu
“Tunataka Hospitali ya Mirembe ifanye kampeni za hamasa na kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya ya akili, matibabu, tafiti mbalimbali za masuala ya afya ya akili pamoja na kufanya mafunzo” amesema Waziri Ummy.