Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam CPA, Amos Makalla amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya Serengeti anaetekeleza Mradi wa Visima vya Maji Kimbiji na Mpela kurudi site mara Moja baada ya mkandarasi huyo kusuasua na kuingia mitini.
CPA, Makalla ametoa maelekezo hayo wakati wa Ziara ya kukagua kama mradi huo unaendelea au umesimama na kuthibitisha pasipokuwa na shaka kuwa Kazi zimesimama kwa muda mrefu.
Kutokana na Hilo, CPA Makalla amemuelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo kuweka kambi kwenye Miradi hiyo na kuhakikisha kazi usafishaji wa Visima inafanyikwa kwa Kasi Ili vikamilike mapema.
Aidha CPA, Makalla ametoa muda wa wiki Moja kwa Bodi na Menejimenti ya DAWASA kumkabidhi mpangokazi wa ujenzi wa miundombinu ya kupokea Maji kutoka kwenye visima hivyo na kuyapeleka kwenye bomba Kuu.
Lengo la CPA Makalla ni kuona DAWASA inakuwa na mbadala wa *Maji ya Dharura yatakayosaidia kipindi Cha miezi ya November na Decembe ambapo kunakuwa na ukame Unaopelekea mgao wa Maji na Mkuu wa Mkoa anaamini visima vya Kimbiji na Mpela vinaweza Kusaidia kupunguza makali ya mgao.
Pamoja na hayo CPA, Makalla amewaelekeza DAWASA kuhakikisha Wananchi wa Kata ya Kisarawe wanafikiwa na huduma ya Maji.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Halima Bulembo na Kaimu mtendaji mkuu wa DAWASA Eng.Shaban Mkwanywe kwa pamoja wamesema utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa utaanza Mara Moja.
Mradi wa Visima vya Maji Kimbiji na Mpela Kigamboni unahusisha visima 20 ambapo kati ya hivyo visima 7 pekee ndio vimekamilika jambo ambalo RC Makalla hakubaliani nalo sababu mradi ulitegemewa kukamilika tokea mwaka 2014.