Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dkt. John Kalage (wa pili kulia) akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo juu ya mapendekezo ya kuzingatiwa katika Upangaji wa Bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Miradi HakiElimu na Meneja Habari na Uchechemuzi HakiElimu, Elisante Kitulo (wa kwanza kulia). |
Na Joachim Mushi, Dar
TAASISI ya HakiElimu imeitaka Serikali kuongeza Bajeti ya Sekta ya Elimu ili kiwango cha fedha inayotengwa iwiane na viwango vilivyopendekezwa na Tamko la Incheoni Juu ya Upangaji wa Bajeti ya Sekta ya Elimu la Mwaka 2015 ambalo Tanzania imeridhia, azimio la Incheon linazitaka nchi zilizo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kutenga walau asilimia 20 ya bajeti kuu za serikali zao kwa ajili ya sekta ya elimu.
Ushauri huo umetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dkt. John Kalage alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam juu ya mapendekezo ya kuzingatiwa katika Upangaji wa Bajeti ya sekta ya elimu kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Dkt. Kalage alisema mpango wa tatu wa Maendeleo ya Elimu (ESDP III) unaainisha vipaumbele na makadirio ya bajeti inayohitajika ili kutekeleza utoaji huduma ya elimu nchini kwa kipindi cha miaka mitano 2021/22-2025/26. Tangu kuanza kwa utekelezaji wa ESDP III, Serikali imeshindwa kuzingatia mapendekezo ya kibajeti kama yalivyoainishwa katika mpango huu.
“…Mfano, wakati ESDP III ilikadiria bajeti ya TZS bilioni 7,116 kwa Mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilitenga na kuidhinisha TZS bilioni 5,645 ambayo ni sawa na asilimia 79.3% ya makadirio. Kwa mwaka 2022/2023 ESDP III iliainisha kiasi cha TZS bilioni 7,587 wakati serikali ilidhinisha na kupitisha TZS 5,729 ambayo ni sawa na asilimia 75.5% ya bajeti iniliyotakiwa kutekeleza mpango.
Akifafanua zaidi, Dk. Kalage aliishauri Serikali kuja na mpango madhubuti na unaopimika wa kutatua changamoto ya miundombinu shuleni, ikiwemo kujenga madarasa angalau 25,000 kwa ajili ya shule za msingi (20,000) na sekondari (5,000) kila mwaka ili ndani ya miaka mitano ijayo tuwe tumetatua changamoto hiyo.
Aidha, alipendekeza kuboreshwa kwa viwango vya Ruzuku kwa Mwanafunzi ili kukabiliana na changamoto ya ongezeko la gharama za maisha na kuamua kuongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka TZS 8,500 kwa siku hadi TZS 10,000.
“…Tunapendekeza viwango vya ruzuku kuongezeka hadi kufikia TZS 25,000 kwa shule za msingi kwa mwanafunzi na TZS 50,000 kwa shule za sekondari. Serikali pia ipitie upya Mwongozo wa utoaji ruzuku ili kuruhusu matumizi ya fedha ya ruzuku katika kutoa huduma ya chakula shuleni pamoja na ununuzi wa SODO kwa watoto wa kike wanaohitaji kujihifadhi nyakati za hedhi. Ikumbukwe pia serikali imeandaa Mwongozo wa Utoaji wa Huduma ya Chakula na Lishe Shuleni. Mwongozo huo unaelekeza utolewaji wa huduma ya chakula shuleni katika viwango stahiki ili kuboresha afya na mahudhurio ya wanafunzi,” alisisitiza Dk. Kalage.
Maeneo mengine aliyoyagusia ni kuwekwa mpango wa kuajiri walimu wa kutosha, kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo na Mitaala ili kupata Sera na Mitaala iliyo bora na inayokidhi mahitaji ya Karne ya 21 na maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla.
HakiElimu imepinga sababu ambayo hutolewa mara kadhaa na Serikali za ufinyu wa bajeti na kuishauri kuboresha zaidi mfumo wa usimamizi wa makusanyo na matumizi ya fedha za umma ili kuondoa udhaifu uliopo.
“..Ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zinaonesha iko mianya mingi ya matumizi na makusanyo mabaya ya fedha za umma ambayo kama itafanyiwa kazi, serikali itapata fedha za kutosha kutoa huduma.
Mathalani, kwa mujibu wa taarifa ya CAG mwaka wa fedha 2021/22; TZS bilioni 88.42 zilizotolewa kama mikopo kwa makundi ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) 180 nchini, hazikurejeshwa.
“Mamlaka 98 hazikuwasilisha kiasi cha TZS bilioni 15.19 zilizokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato na TZS bilioni 8.99 zilikopeshwa na Halmashauri lakini hazikurejeshwa. Ripoti hiyo inaonesha pia Mamlaka za Serikali za Mtaa kushindwa kukusanya TZS 76.56 bilioni walizotakiwa kukusanya kutokana na mapato ya vizimba, tozo, ushuru na leseni kama ilivyotarajiwa.” Alisema na kuongeza kuwa pamoja na maeneo mengine yenye udhaifu wa kupoteza mapato kama hayo yakifanyiwa kazi Serikali itapata fedha za kutosha kutoa huduma.